Ballon d'Or 2021: Messi ashinda tuzo la mchezaji bora kwa mara ya 7, Chelsea yatuzwa kama klabu bora

Muhtasari

•Kinyang'anyiro kikubwa kilikuwa kati ya Messi na mshambulizi wa Bayern Munich Robert Lewandowski ambaye pia alikuwa amependekezwa sana kupokea tuzo la mwaka huu

•Klabu ya Chelsea ambayo ilikuwa na wachezaji watano waliopendekezwa kupokea tuzo la Ballon d'Or ilitambuliwa kama klabu bora ya mwaka .wa 2021 

Messi apokea tuzo la mchezaji bora kwa mara ya 7
Messi apokea tuzo la mchezaji bora kwa mara ya 7
Image: BALLON D'OR TWITTER

Hafla ya kutuza wababe wa soka mwaka wa 2021 ilifanyika usiku wa kuamkia Jumanne katika ukumbi wa Chartelet Theatre jijini Paris, Ufaransa.

Mshambulizi matata wa Paris Saint-Germain, Lionel Andre Messi alipokea tuzo la mchezaji bora wa mwaka wa 2021 almaarufu kama Ballon d'Or kwa mara nyingine na kufikisha idadi ya tuzo za mchezaji bora wa mwaka  zilizo kwenye kabati yake kuwa saba.

Kinyang'anyiro kikubwa kilikuwa kati ya Messi na mshambulizi wa Bayern Munich Robert Lewandowski ambaye pia alikuwa amependekezwa sana kupokea tuzo la mwaka huu. Jorginho wa Chelsea aliibuka wa tatu.

Mzaliwa huyo wa Argentina mwenye umri wa miaka 34 alishinda tuzo hilo tena mwaka wa 2009, 2010, 2011, 2012, 2015 na 2019.

Tuzo la mwaka wa 2020 lilifutwa kufuatia janga la Corona lakini wengi walitarajia Lewandowski alipokee.

Kiungo wa timu ya wanawake ya Barcelona Alexia Putellas alishinda tuzo la Ballon d'Or 2021 upande wa wanawake. Jennifer Hermoso wa Barcelona na Sam Kerr wa Chelsea waliibuka wa pili na wa tatu mtawalia

Mlinda lango wa PSG Gigi Donnarumma alipokea tuzo la mlinda lango wa mwaka almaarufu kama Yashin Trophy kufuatia ubabe wake katika mashindano ya Euro 2020 na  msimu mzuri uliopita na klabu yake ya awali AC Milan

Lewandoski hakutoka mkono bure kwani alipokea tuzo la mshambulizi bora wa mwaka kwa kuwa mfungaji mabao bora katika klabu yake na nchi.

Pedri wa Barcelona alishinda tuzo la mchezaji bora chini ya umri wa miaka 21 akifuatwa na Jude Bellingham wa Borrusia Dortmund na Jamal Musiala wa Bayern Munich

Klabu ya Chelsea ambayo ilikuwa na wachezaji watano waliopendekezwa kupokea tuzo la Ballon d'Or ilitambuliwa kama klabu bora ya mwaka .wa 2021