Wachezaji wa zamani wataka kusimamia soka Kenya

Muhtasari

• Shollei alisema wachezaji wengi wanashikilia uaminifu wa vilabu na ushindani kutoka siku zao wakicheza na hivyo hawawezi kufanya kazi pamoja kubadilisha soka ya humu nchini.

• Shollei, ambaye pia alidokeza kuwania urais wa FKF wakati uchaguzi utakapoitishwa, aliomba Kamati ya Wasimamizi kutoa utratibu wa uchaguzi.

Sammy Shollei (C) akiwa na mchezaji wa zamani wa Harambee Stars Kennedy Ambundo na Fred Ngawo Picha: EMMANUEL SABUNI
Sammy Shollei (C) akiwa na mchezaji wa zamani wa Harambee Stars Kennedy Ambundo na Fred Ngawo Picha: EMMANUEL SABUNI

Kiungo wa zamani wa Harambee Stars Sammy Shollei anaamini kwamba vuta ni kuvute kati ya waliokuwa wachezaji ndio sababu kuu ya mpira wa kandanda kutekwa nyara na watu wasio waaminifu wanaotaka kusambaratisha soka nchini.

Shollei alisema wachezaji wengi wanashikilia uaminifu wa vilabu na ushindani kutoka siku zao wakicheza na hivyo hawawezi kufanya kazi pamoja kubadilisha soka ya humu nchini.

“Nimejaribu mara nyingi kuleta wachezaji wa zamani kwenye shirikisho na si rahisi kwa sababu bado tuna utamaduni wa nani alichezea timu gani. Wachezaji wa AFC Leopards na Gor Mahia hawako na uhusiano mema na  wale waliochezea Kenya Breweries ( kwa sasa Tusker) wao hujiona kama wasomi, kuliko wengine jambo ambalo si kweli,” mchezaji huyo wa zamani wa Kenya Breweries alisema.

Njia moja ya kuleta mabadiliko kwenye mchezo huo, Shollei anaamini, ni wachezaji wa zamani kugombea nyadhifa na kuwafurusha wapiga debe wanaozorotesha soka ya humu nchini na kusambaratisha ndoto za vijana wengi wenye vipaji.

"Hakuna mtu asiye mwaminifu ambaye atataka kufanya kazi na wachezaji wa zamani kwa sababu sisi ni watu walionyooka sana. Mashariki au Magharibi, watakukabili na kukuambia ukweli. Ukikosea watakukabili na kukueleza mengi,” Shollei alisema.

Alidai kwamba wachezaji wengi wa zamani wanaogopa vita ambavyo mara nyingi huambatana na chaguzi hivyo basi wengi hujitenga na chaguzi hizo.

"Utamaduni wetu siku zote umekuwa kufurahisha mashabiki, sio kufanya siasa. Wakati wowote mtu anapoanzisha vita, anatufokea, au anatumia maneno fulani ya kisiasa, tunaogopa na kujikalisha pembeni. Si hulka yetu kupiga kelele na ndiyo maana wengi wanahepa usimamizi wa soka,” alisema.

Shollei, hata hivyo, aliwataka wachezaji wa zamani kuchukua nyadhifa katika usimamizi wa soka ikiwa Kamati ya Waangalizi ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) inataka uchaguzi ufanyike haraka iwezekanavyo.

Shollei, ambaye pia alidokeza kuwania urais wa FKF wakati uchaguzi utakapoitishwa, aliomba Kamati ya Wasimamizi kutoa utratibu wa uchaguzi.