Afcon 2021: Ivory Coast yamuita kikosini wing'a wa Crystal Palace Wilfried Zaha

Muhtasari
  • Ivory Coast yamuita kikosini wing'a wa Crystal Palace Wilfried Zaha

Mshambulizi wa Crystal Palace Wilfried Zaha amejumuishwa katika kikosi cha Ivory Coast kitakachoshiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Cameroon.

Shaka ilikuwepo juu ya mustakabali wa nyota huyo kimataifa mwenye umri wa miaka 29 mwezi uliopita baada ya kuripotiwa kuomba kutojumuishwa katika mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia mwezi Novemba.

Hata hivyo, meneja wa Palace Patrick Vieira alisisitiza Zaha alitaka kuendelea kuichezea The Elephants.

Beki wa Manchester United Eric Bailly pia yuko kwenye kikosi cha wachezaji 28, lakini hakuna nafasi kwa mchezaji mwenzake wa klabu hiyo Amad Diallo.

Winga Diallo, 19, ameichezea United mara moja tu msimu huu - katika sare ya 1-1 na Young Boys ya Uswizi katika mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mnamo 8 Desemba.

Kocha wa Ivory Coast Patrice Beaumelle alisema mnamo Agosti anatumai kwamba Diallo ataweza kutoka kwa mkopo ili kupata nafasi zaidi ya kucheza.

Beaumelle atatumaini kuwa kiwango kizuri cha Sebastien Haller kinaweza kuendelea, huku mshambuliaji huyo wa Ajax na wa zamani wa West Ham akiwa na msimu uliovunja rekodi kwenye Ligi ya Mabingwa, akifunga mabao 10 hadi sasa.

Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa Maxwel Cornet anaweza kuwa mchezaji mwingine muhimu baada ya kuonesha kiwango kizuri katika klabu ya Burnley ya Ligi Kuu ya Uingereza msimu huu. Beki wa Wolves Willy Boly, kiungo wa kati wa Fulham Jean Michael Serri na mshambuliaji wa Arsenal Nicolas Pepe pia wamejumuishwa.

Wachezaji wanne kutoka Italia wamo kwenye orodha hiyo huku Franck Kessie wa AC Milan na Jean-Daniel Akpa Akpro wa Lazio wakiungana na nyota wa Sassuolo Hamed Traore na Jeremie Boga.

Ivory Coast, ambao walishinda taji la pili kati ya mawili ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka wa 2015, wanaanza kampeni yao ya Kundi E nchini Cameroon dhidi ya Equatorial Guinea tarehe 12 Januari kabla ya kucheza na Sierra Leone na mabingwa watetezi Algeria.