EPL 2021/22: Matokeo ya raundi ya 19

Muhtasari

•Mechi tatu ambazo zilipaswa kuchezwa siku ya Jumapili ziliahirishwa kufuatia ongezeko la visa vya Covid 19 miongoni mwa wachezaji. 

Image: INSTAGRAM// ARSENAL

Michuano ya EPL 2021/22 bado  inaendelea huku ikiingia katika raundi ya 19 wikendi  iliyotamatika ya Krismasi.

Jumla ya mechi sita zilichezwa katika viwanja mbalimbali nchini Uingereza siku ya Jumapili. Michuano tatu ya kwanza ilichezwa mwendo wa saa kumi na mbili jioni.

Mabingwa watetezi wa kombe la  EPL Manchester City walikaribisha washindi wa EPL 2015/16 Leicester City katika uga wao wa Etihad ambapo walipimana nguvu katika mechi iliyoshuhudia mabao mengi mno.

Vijana wa Pep Guardiola walipata ushindi mkubwa wa 6-3. Kelvin De Bruyne, Riyad Mahrez, Ikay Gundogan, Aymeric Laporte na  Raheem Sterling walifanikisha ushindi huo kwa bao moja kila mmoja. James Maddison, Ademola Lookman na Kelechi Ihenacho ndio walifunga mabao ya Leicester.

Wanabunduki waliendeleza fomu yao nzuri huku wakipata ushindi wa tano mfululizo katika mashindano yote ambayo wanashiriki.

Safari yao ya Carrow Road kumenyana na Norwich City ilikuwa yenye mafinikio huku wakirejea nyumbani na pointi zote tatu baada ya kufunga mabao 5 bila jawabu. Mabao mawili ya Bukayo Saka na bao mojamoja ya Kieran Tierney, Alexandre Lacazette na Emile Smith Rowe yalifanikisha ushindi huo.

Tottenham walipata ushindi wa 3-0 nyumbani dhidi ya Crystal Palace. Harry Kane na Lucas Moura walitangulia kwa kufunga katika dakika ya 32 na 34 mtawalia.

Palace walilazimika kukamilisha mechi na wachezaji 10 pekee baada ya mshambulizi matata Wilfred Zaha kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 37. Son Heung-Min aliongeza machungu kwenye kidonda cha wageni huku akifunga bao la kufunga mechi katika dakika ya 74.

Southampton walizima West Ham ugenini kwa mabao 3-2 na kuboresha nafasi yao katika jedwali. 

Aston Villa walipoteza nyumbani dhidi ya Chelsea licha ya kutangulia kufunga kupitia bao la kujifunga la Recce James katika dakika ya 28. Penalti mbili za Jorginho na bao la Romelu Lukaku zilifanikisha ushindi wa The Blues.

Mechi ya mwisho siku ya Jumapili ilikuwa kati ya Brighton na Brentford ambapo wenyeji walinyakua pointi zote tatu baada ya kuwafunga wageni wao mabao mawili bila jawabu. Leandro Trossard na Neal Maupay ndio walifungia Brighton.

Mechi tatu ambazo zilipaswa kuchezwa siku ya Jumapili ziliahirishwa kufuatia ongezeko la visa vya Covid 19 miongoni mwa wachezaji. Mechi zilizoathirika ni ile kati ya Liverpool na Leeds, Wolves dhidi vs Watford na Burnley vs Everton.

Newcastle watawakaribisha Manchester United ugani St James Park usiku wa leo (Jumatatu)