'Ni wakati mwafaka wa mabadiliko!' Anthony Martial aiambia United anataka kuondoka

Muhtasari

•Licha ya kutaka kuondoka Old Trafford, Rangnick alithibitisha kuwa klabu hiyo bado haijapokea ofa ya kumnunua fowadi huyo.

Mshambulizi Anthony Martial
Mshambulizi Anthony Martial
Image: GETTY IMAGES

Mshambulizi Mfaransa Anthony Martial amemwambia meneja wa muda wa Manchester United Ralf Rangnick anataka kuondoka.

Rangnick alisema "alizungumza kwa kirefu" siku ya Jumatano na kijana huyo mwenye umri wa miaka 26, ambaye alimwambia "ni wakati mwafaka wa mabadiliko".

Martial ameanza mechi mbili pekee za Premier League msimu huu, akifunga mara moja.

Licha ya kutaka kuondoka Old Trafford, Rangnick alithibitisha kuwa klabu hiyo bado haijapokea ofa ya kumnunua fowadi huyo.

Wakala wa mchezaji huyo Philippe Lamboley alithibitisha mapema mwezi huu Martial alitaka kuondoka katika klabu hiyo mwezi Januari, na kuongeza kuwa "atazungumza na klabu hivi karibuni".

Rangnick alisema: "Alinieleza kuwa amekuwa Manchester United sasa kwa miaka saba iliyopita na anahisi ni wakati mwafaka wa mabadiliko, kwenda mahali pengine."

Martial alisajiliwa na United mwaka 2015 kutoka Monaco kwa £36m, na kumfanya kuwa mwanasoka ghali zaidi duniani wakati huo.

Amefunga mabao 79 katika mechi 268 akiwa na Mashetani Wekundu lakini amekuwa mchezaji wa pembeni kufuatia kuwasili kwa Cristiano Ronaldo, Edinson Cavani na Jadon Sancho.

Hajashiriki katika mechi yoyote ya Rangnick kama kocha hadi sasa na amecheza mechi 10 pekee katika mashindano yote msimu huu.

"Nadhani kwa njia inaeleweka," aliongeza Rangnick.

"Ningeweza kufuata mawazo yake lakini kwa upande mwingine, ni muhimu pia kuona hali ya klabu. Tuna nyakati za Covid, tuna mashindano matatu ambayo tuna matarajio makubwa na tunataka kuwa na mafanikio kadri tuwezavyo.

"Hadi sasa, nijuavyo, hakujawa na ofa yoyote kutoka kwa klabu nyingine yoyote na mradi iwe hivi atabaki."

'Hali ya chanjo inaweza kuzingatiwa kwa wasajili wapya'

Rangnick pia alisema na wasiwasi kama wa meneja wa Liverpool Jurgen Klopp juu ya kusajili wachezaji ambao hawajachanjwa dhidi ya coronavirus.

Hivi majuzi Klopp alisema hadhi ya mchezaji kupata chanjo itakuwa na "mvuto" katika uamuzi wa klabu kuwasajili.

"Nadhani inaweza kuwa jambo la kuzingatia," Rangnick alisema.

"Hili ni suala ambalo vilabu vinapaswa kulifikiria kwa umakini. Ukisajili mchezaji ukijua tangu siku ya kwanza hajapata chanjo, unapaswa kufahamu kuwa huenda hapatikani."

"Sio kwa siku 10 tu, lakini hii inaweza kutokea mara kwa mara katika nyakati za Covid."

United ililazimika kufunga sehemu ya kikosi cha kwanza cha kituo chao cha Carrington kwa sababu ya mlipuko wa Covid na wameahirisha michezo miwili ya Ligi Kuu mnamo Desemba.

Ligi ya Premia ilisema 84% ya wachezaji wako kwenye "safari yao ya chanjo" kulingana na takwimu za hivi karibuni, na kuacha 16% bila chanjo.

Takwimu zinalingana na vikundi vya umri vinavyolingana katika jamii nchini Uingereza.

Rangnick alitumia mfano wa Joshua Kimmich wa Bayern Munich kama ushahidi kwamba wachezaji wanapaswa kupata chanjo haraka iwezekanavyo.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani, 26, hivi majuzi alisema anajuta kutopewa chanjo baada ya kupata tatizo la mapafu kutokana na Covid-19.

"[Kimmich] alisitasita sana mwanzoni na nadhani kwa wakati huo amegundua kuwa inaweza kuwa wazo zuri kupata chanjo," Rangnick aliongeza.

"Alimshika Covid na bado ana matatizo katika mapafu yake. Nadhani hili ni suala ambalo bila shaka kila mtu anaweza, na anapaswa kuwa na hiari yake. Lakini katika soka, hasa katika kiwango hiki tunachocheza, tunahitaji kujaribu. kuwashawishi wachezaji wetu kupata chanjo.

"Inapaswa kuwa kwa maslahi ya wachezaji kupata chanjo, lakini mwishowe ni uamuzi ambao kila klabu inapaswa kuchukua yenyewe na kutafuta suluhisho bora zaidi."