Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yaliyokuwa yamesubiriwa kwa hamu hatimaye yalianza rasmi siku ya Jumapili.
Mashindano hayo ambayo hufanyika kila baada ya miaka miwili yataendelea kwa kipindi cha takriban mwezi mmoja hadi Februari 6 wakati ambapo fainali itachezwa.
Kombe hilo limejumuisha mataifa 24 ya Afrika. Harambee Stars ya Kenya hata hivyo haikuweza kufuzu kushiriki katika kombe hilo.
Jumla ya mechi mbili zilichezwa katika siku ya kwanza ya Afcon.
Washindi wa AFCON mara tano Cameroon na ambao pia ni waandaji wa kombe hilo walimenyana na Burkina Faso mwendo wa saa moja jioni.
Burkina Faso ilitangulia kufunga katika dakika ya 24 kupitia kiungo Gustavo Sangare kabla ya mshambulizi Vincent Aboubakar kufungia wenyeji mikwaju miwili ya penalti katika dakika ya 40 na 45+3.
Mechi ya pili kati ya Ethiopia na Cape Verde ilichezwa mwendo wa saa nne usiku.
Ethiopia ililazimika kucheza bila mchezaji mmoja kwa zaidi ya dakika 80 baada ya mlinzi Yared Bayeh kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 12.
Mshambulizi Julio Tavares alifungia Cape Verde bao la pekee katika dakika ya 45 na kusaidia taifa lake kunyakua pointi zote tatu.
Mechi nne zaidi zinatarajiwa kuchezwa siku ya Jumatatu.