Tatizo la moyo lamlazimu Aubameyang kuondoka Afcon mapema

Muhtasari

•Raia huyo wa Gabon mwenye umri wa miaka 32 aliondoka katika kambi ya timu yake ya taifa siku ya Jumatatu na kurudi London ili kufanyiwa vipimo zaidi vya kiafya.

Mshambulizi wa Arsenal na Gabon Pierre Emerick Aubameyang
Mshambulizi wa Arsenal na Gabon Pierre Emerick Aubameyang
Image: HISANI

Mshambulizi matata wa klabu ya Arsenal, Pierre Emerick Aubameyang amelazimika kukatiza safari yake ya AFCON baada ya kugunduliwa kuwa na vidonda vya moyo siku kadhaa tu baada ya kuugua Covid 19.

Raia huyo wa Gabon mwenye umri wa miaka 32 aliondoka katika kambi ya timu yake ya taifa siku ya Jumatatu na kurudi London ili kufanyiwa vipimo zaidi vya kiafya.

Shirikisho la soka la Gabon limethibitisha kwamba Aubameyang hatashirikishwa tena katika kikosi cha taifa hilo kwani tayari amepatiwa ruhusa kurudi Arsenal kwa masuala ya kiafya.

"Shirikisho la Soka la Gabon limeamua kuwarejesha wachezaji Pierre-Emerick Aubameyang na Mario Lemina katika vilabu vyao ili wafanyiwe mitihani zaidi ya afya" Shirikisho hilo lilisema katika taarifa fupi.

Aubameyang pamoja na mwenzake Mario Lemina wa Nice hawajashiriki katika mechi yoyote ya Afcon tangu kombe hilo lilipoanza baada ya kupatikana na virusi vya Corona siku chache kabla ya mechi ya kwanza ya Gabon.

Wawili hao wamekosa mechi mbili za Gabon ambapo timu hiyo imeandikisha sare ya 1-1 na ushindi wa 1-0 dhidi ya Ghana na Comoros mtawalia.