Christian Eriksen arejea EPL miezi 7 baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo akiwa uwanjani

Muhtasari

•Brentford ilitangaza usajili wa Eriksen Jumatatu asubuhi huku ikieleza kwamba mchezaji huyo atajiunga rasmi na klabu baada yake kupata kibali cha kimataifa.

•Aliondoka Inter Milan mnamo mwezi Desemba mwaka jana kufuatia makubaliano ya pamoja kwani kifaa alichowekwa moyoni kilimaanisha hangeweza kuendelea kucheza Italia.

Christian Eriksen asajiliwa na Brentford
Christian Eriksen asajiliwa na Brentford
Image: BRENTFORD

Kiungo Christian Eriksen amesajiliwa na klabu ya Brentford miezi saba tu baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo na kuzirai akiwa uwanjani wakati wa mashindano ya EURO 2020.

Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Denmark ametia saini mkataba mfupi wa miezi sita na klabu hiyo ambayo ilirejea Ligi Kuu msimu huu.

Brentford ilitangaza usajili wa Eriksen Jumatatu asubuhi huku ikieleza kwamba mchezaji huyo atajiunga rasmi na klabu baada yake kupata kibali cha kimataifa.

Meneja Thomas Frank amesema anatazamia kufanya kazi tena na mchezaji huyo ambaye alifunza miaka michache iliyopita katika timu ya wachezaji wadogo ya Udenmarki.

""Tumechukua fursa ya kushangaza kuleta mchezaji matata  duniani. Hajafanya mazoezi na timu kwa miezi saba lakini amefanya kazi nyingi peke yake. Yuko fiti lakini tutahitaji kumfanya awe fiti zaidi na ninatazamia kumuona akifanya kazi na wachezaji na wafanyakazi ili kurejea kwenye kiwango chake cha juu zaidi," Frank alisema.

Eriksen kwa upande wake ameeleza furaha yake kujiunga na Brentford huku akisema anatazamia sana kuanza kushiriki katika mechi.

Mchezaji huyo aliondoka Inter Milan mnamo mwezi Desemba mwaka jana kufuatia makubaliano ya pamoja kwani kifaa alichowekwa moyoni kilimaanisha hangeweza kuendelea kucheza Italia.

Alipatwa na mshtuko wa moyo na kuzirai uwanjani wakati wa mechi ya Denmark dhidi ya Finland katika mashindano ya EURO yaliyofanyika mapema  mwaka jana.