United yamsimamisha Mason Greenwood kufuatia madai ya ubakaji na unyanyasaji wa kinyumbani

Muhtasari

•United imetangaza kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 hatarejea kwenye mazoezi au mechi kwa kipindi kisichodhihirika.

•Mwanamume mwenye umri wa miaka 20 ambaye anaaminika kuwa mshambulizi huyo alikamatwa Jumapili kufuatia tuhuma za ubakaji na unyanyasaji.

Mshambulizi wa United Mason Greenwood ashtumiwa kwa kosa la unyanyasaji wa kinyumbani
Mshambulizi wa United Mason Greenwood ashtumiwa kwa kosa la unyanyasaji wa kinyumbani
Image: HISANI

Klabu ya Manchester United imemsimamisha kazi mshambulizi wake Mason Greenwood kufuatia madai ya ubakaji na unyanyasaji wa kinyumbani yanayomkabili.

United imetangaza kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 hatarejea kwenye mazoezi au mechi kwa kipindi kisichodhihirika.

Katika taarifa ya hapo awali, klabu hiyo iliweka wazi kuwa wanafahamu kuhusu  "picha na madai" ambayo yalionekana kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mshambulizi huyo.

Mmoja wa wasemaji wa klabu alissisitiza kwamba klabu hiyo "haikubaliani na vurugu za aina yoyote"

Ripoti kutoka Uingereza zinasema kuwa mwanamume mwenye umri wa miaka 20 ambaye anaaminika kuwa mshambulizi huyo alikamatwa Jumapili kufuatia tuhuma za ubakaji na unyanyasaji.

Taarifa ya polisi kutoka Greater Manchester ilisema kwamba wanafahamu kuhusu picha na video zilizopakiwa na mwanadada mmoja akiripoti kunyanyaswa.

"Uchunguzi ulianzishwa na kufuatia uchunguzi tunaweza kuthibitisha kuwa mwanamume mwenye umri wa miaka 20 amekamatwa kwa tuhuma za ubakaji na unyanyasaji. Anaendelea kuzuiliwa kwa mahojiano. Uchunguzi unaendelea." Taarifa hiyo ilisoma.

Mshambulizi huyo ambaye alianza kuchezea Mashetani Wekundu mwaka wa 2019 bado hajatoa taarifa yoyote kuhusiana na tuhuma hizo.