Morrison aomba radhi Simba

Muhtasari

• Hatimaye mchezaji winga wa klabu ya Simba kutoka Tanzania Mghana Benard Morrison ameomba radhi uongozi wa timu hiyo.

• Morrison alifurushwa kutoka kambi ya mazoezi ya timu ya Simba mwishoni mwa wiki jana kwa tuhuma za utovu wa nidhamu

Benard Morrison
Image: Facebook

Baada ya vuta nikuvute ya wiki moja, hatimaye mchezaji winga wa klabu ya Simba kutoka Tanzania Mghana Benard Morrison ameomba radhi uongozi wa timu hiyo.

Morrison alifurushwa kutoka kambi ya mazoezi ya timu ya Simba mwishoni mwa wiki jana kwa tuhuma za utovu wa nidhamu na akatakiwa kuandika barua ya maelezo kwa Afisa Mtendaji Mkuu Barbara Gonzalez ila akadinda kuandika barua kwa kusisitiza kwamba hana makosa ya aina yoyote, jambo ambalo liliuweka uongozi wa timu hiyo kwenye njia panda pasi na kujua la kufanya.

Morrison ambaye alijiunga na timu ya Simba mwaka wa 2020 baada ya kandarasi yake na Yanga kukamilika amekuwa ni nguzo muhimu kwa wekundu wa msimbazi ila tuhuma za kukosa nidhani akiwa mazoezini zilisababisha kusimamishwa kwa muda na baadae kutakiwa kuandika barua ya kujieleza kuhusiana na tuhuma dhidi yake.

Taarifa zinasema kwamba baada ya tathmini ya muda, Morrison ameandika ujumbe wa kuomba radhi kwenye kundi la mtandao wa WhatsApp ya wachezaji wa timu hiyo na pia kutuma nakala ingine kwa kiongozi wa timu.

Morrison amekuwa ni tegemeo la kusakanya mabao kwa upande wa Simba tangu kujiunga nao na msimu uliopita alikuwa miongoni wa kikosi kilichoshinda taji la ligi kuu bara, na pia kuisaidia timu hiyo kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Mpaka sasa haijulikani ni nini hatimaye yake na klabu ya Simba baada ya msamaha huo na wala haijulikani uongozi wa timu utaupokelea vipi msamaha wake ila inadaiwa hawezi tena kurudishwa kikosini.

Nini cha mno kwa mchezaji Benard Morrison?