Beki wa Manchester City Joao Cancelo na familia yake wavamiwa na wezi

Muhtasari

•Cancelo, mwenye umri wa miaka 27, alijeruhiwa usoni baada ya kujaribu kupambana na kundi la wezi hao wanne waliovamia nyumbani kwake mwezi Disemba.

Crime Scene

Mlinzi wa Manchester City Joao Cancelo amezungumzia tukio la "kutisha" la kuvamiwa na wezi alilolielezea "lilitishia familia yangu" na kumjeruhi.

Cancelo, mwenye umri wa miaka 27, alijeruhiwa usoni baada ya kujaribu kupambana na kundi la wezi hao wanne waliovamia nyumbani kwake mwezi Disemba.

"Familia yangu haistahili kupitia ilichokipitia," alisema nyota huyo wa kimataifa wa Ureno, akizungumza na vyombo va habari kwa mara ya kwanza kuhusu tukio hilo.

"Ni maisha, inatokea kwenye maisha. Napaswa kusonga mbele."

Cancelo aliweza kucheza katika mcheo ambao City walishinda 2-1 dhidi ya Arsenal mnamo 1 Januari - siku mbili baada ya tukio hilo. Alipimwa na jopo la matabibu na kuonekana anaweza kucheza mchezo huo.

Aliweka kwenye mtandaoni wa Instagram picha kuonyesha majeraha yake saa chache tu baada ya tukio hilo la kutisha.

"Kwa bahati mbaya leo nilivamiwa na watu wanne ambao waliniumiza na kujaribu kuumiza familia yangu," aliandika.

"Unapoonyesha upinzani, ndivyo inavyotokea. Walifanikiwa kuchukua vito vyangu vyote na kuniacha na uso wangu na hali hii."

Licha ya shambulio hilo, Cancelo amekuwa akionyesha kiwango bora kwenye timu yake ya Man City ambapo amekuwa akicheza zaidi upande wa kulia au kushoto wa ulinzi.

Mapema mwezi huu alisaini mkataba mpya wa miaka mitano na vinara hao wa Ligi Kuu ya England, kusalia Etihad hadi mwaka 2027.