Shirikisho la soka duniani Fifa, limeifungia Kenya dhidi ya kushiriki katika mashindano yote ya kimataifa.
Zimbabwe pia ilikumbwa na hali kama hiyo huku rais wa Fifa Gianni Infantino akizikemea serikali za nchi hizo mbili kwa kuingilia shughuli za soka, kinyume na sheria za Fifa.
"Ilitubidi tusimamishe wanachama wetu wawili - Kenya na Zimbabwe. Wote kwa kuingiliwa na serikali katika shughuli za shirikisho la soka,” Infantino alisema Alhamisi jioni.
"Wanachama hawa wawili wamesimamishwa kufanya shughuli za soka mara moja na wanajua wanachopawa kufanya ili waruhusiwe kurejea au adhabu hiyo kuondolewa." Alisema.
Hatua hiyo inajiri wiki moja tu baada ya timu ya taifa ya wanawake Harambee Starlets kuondolewa katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake dhidi ya Uganda ambayo ilikuwa imepangwa kuchezwa Februari 17.
Barry Otieno ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji katika shirikisho lililovunjwa aliandika barua kwa bodi inayosimamia soka barani Afrika, Caf, akitaka Starlets kuondolewa kwenye mashindano hayo.
Masaibu yalianza mnamoNovemba 11, wakati waziri wa michezo Amina Mohamed alipovunja bodi ilioyongozwa na Nick Mwendwa na kuteua kamati ya muda kusimamia shughuli za soka nchini.
Jaji Mstaafu Aaron Ringera aliteuliwa kuongoza kamatihiyo ya wanachama 15 ambayo ingehudumu kwa miezi sita.
Wengine walioteuliwa kwenye kamati hiyo ni Jenerali Mstaafu Moses Oyugi, Fatma Adan, Philip Musyimi, Anthony Isayi, Elisha Kiplagat na Hassan Haji, Fredrick Tureisa, Mwangi Muthee, Neddy Atieno, Ali Amour, Titus Kasuve, Richard Omwela, Bobby Ogolla na JJ. Masiga.
Waziri alichukua hatua hiyo baada ya kupokea ripoti ya ukaguzi kuhusu FKF kutoka kwa Msajili wa Michezo Rose Wasike.