Fifa na Uefa zapiga marufuku klabu za Urusi na timu ya taifa kushiriki mashindano yote

Muhtasari

•Siku ya Jumatatu Fifa na Uefa ziliafikia uamuzi wa kupiga marufuku timu na klabu hizo za Urusi kwa kipindi kisichothibitishwa.

•Shirikisho hizo zinazosimamia soka duniani na Ulaya zilisema kuwa hatua hiyo imechukuliwa kwa mshikamano na watu wote walioathirika nchini Ukraine.

Image: RUSSIAN FOOTBALL TEAM

Vilabu vya soka vya  Urusi pamoja na timu za taifa za nchi hiyo hazitashiriki katika mashindano yoyote ya Fifa na Uefa kwa kipindi kisichojulikana kufuatia uvamizi wa nchi hiyo nchini Ukraine.

Siku ya Jumatatu Fifa na Uefa ziliafikia uamuzi wa kupiga marufuku timu na klabu hizo za Urusi kwa kipindi kisichothibitishwa.

Hatua hii inamaanisha kuwa timu ya taifa ya Urusi ya wanaume haitacheza mechi zao za mchujo za Kombe la Dunia mwezi ujao na timu ya wanawake haitashiriki mashindano ya EURO 2022.

Timu ya wanaume ya Urusi ilitarajiwa kucheza  mechi ya mchujo dhidi ya Poland tarehe 24 mwezi Machi.

Spartak Moscow ya Urusi pia imeondolewa kutoka ligi ya Europa na mshindani wake katika raundi ya 16 RB Leipzig atahitimu kuingia robo fainali.

Uefa pia imesitisha mkataba wake wa udhamini na kampuni ya Gazprom ya Urusi.

Shirikisho hizo zinazosimamia soka duniani na Ulaya zilisema kuwa hatua hiyo imechukuliwa kwa mshikamano na watu wote walioathirika nchini Ukraine.

Timu ya Manchester United pia imesitisha mkataba wake wa udhamini na kampuni ya ndege ya Urusi Aeroflot.