Raila awataka polisi kuwacha kuhangaisha bodaboda kwa makosa ya wachache

Muhtasari

• Kinara wa ODM Raila Odinga sasa anawataka maafisa wa polisi kuwacha kuhangaisha wahudumu wa boda boda.

• Kulingana na Raila, waliohusika katika kisa hicho cha kuvunja moyo wanafaa kukabiliwa na sheria.

KInara wa ODM Raila Odinga
Image: George Owiti

Kinara wa ODM Raila Odinga sasa anawataka maafisa wa polisi kuwacha kuhangaisha wahudumu wa boda boda.

Matamshi yake yanajiri siku chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuagiza msako wa kitaifa katika sekta hiyo.

Raila alionya dhidi ya wahudumu wa bodaboda kudhulumiwa kwa makosa ya wachache kati yao waliomdhulumu mwanamke katika barabara ya Wangari.

Mapema wiki hii, video ilisambaa mitandaoni ya kisa cha wiki jana ambapo kundi la waendesha bodaboda walimvamia na kumdhulumu dereva wa kike jijini Nairobi baada ya ajali.

Raila aliwaambia polisi wakome kuwahangaisha wahudumu wote na badala yake wawatambue na kuwafikisha mahakamani wale watundu.

Kulingana na Raila, waliohusika katika kisa hicho cha kuvunja moyo wanafaa kukabiliwa na sheria.

“Kulikuwa na kisa Nairobi ambapo mwanamke alishambuliwa na waendeshaji Bodaboda, lazima sote tukemee tabia hiyo. Iwapo mtu atafanya makosa ambayo ni mhalifu na anafaa kukabiliwa kisheria, wasiwahangaishe waendeshaji wote,” Raila alisema.

Aliongeza: "Yeyote aliyefanya hivyo atakabiliwa na sheria lakini isiwe lawama kwa sekta nzima. Polisi hawapasi kuwanyanyasa wahudumu wote kwa makosa ya wengine”.