Thiery Henry afunguka kuhusu msongo wa mawazo baada ya kugura Arsenal

Muhtasari

•Wakati huo, Mfaransa huo alikuwa anapambana na jeraha la muda mrefu na alikuwa kwenye harakati ya kutengana na aliyekuwa mkewe Claire Merry.

•Henry alifichua ilimchukua zaidi ya mwaka mmoja kutulia Barcelona kutokana na yale ambayo alikuwa anapitia.

Mshambulizi wa zamani wa Arsenal na Ufaransa
Mshambulizi wa zamani wa Arsenal na Ufaransa
Image: REUTERS

Mwanasoka wa zamani Thierry Henry amefunguka kuhusu alivyoathirika kisaikolojia baada ya kugura klabu ya Arsenal takriban miaka 15 iliyopita.

Mnamo mwaka wa 2007 Henry alijiunga na Barcelona baada ya kuchezea The Gunners kwa zaidi ya mwongo mmoja.

Wakati huo, Mfaransa huo alikuwa anapambana na jeraha la muda mrefu na alikuwa kwenye harakati ya kutengana na aliyekuwa mkewe Claire Merry.

Henry alilazimika kulipa mkewe zaidi ya pauni milioni kufuatia talaka yao iliyokuja takriban miaka mitano tu baada ya kufunga ndoa. Wawili hao walikuwa na binti mmoja pamoja.

Akiwa kwenye mahojiano na L'Equipe, Henry alifichua ilimchukua zaidi ya mwaka mmoja kutulia Barcelona kutokana na yale ambayo alikuwa anapitia.

"Nilipoondoka Arsenal kwenda Barcelona ilinichukua mwaka mmoja kuwa sawa.  Nilifika nikiwa na jeraha na nilikuwa katika harakati ya talaka, lazima ningejifunza mfumo mpya, yote hayo yalifanya nichangikiwe akili," Alisema.

Gwiji huyo wa timu ya taifa ya Ufaransa alisema wakati huo ilikuwa ngumu kufunguka kuhusu hali ya kisaikolojia.

Henry hakuwa kutoa mchango mkubwa sana pale Barcelona kama ilivyokuwa akiwa Arsenal. Hata hivyo aliweza kunyakua vikombe viwili vya Laliga na Champions League moja akiwa na mabingwa hao wa Uhispania.

Aliondoka Barca mwaka wa 2010 na kujiunga na New York Red Bulls ya Marekani.