Kizaazaa chashuhudiwa katika mechi ya Everton baada ya mwandamanaji kujifunga kwenye lango

Muhtasari

• Mwanaume huyo anayetajwa kutumwa na kundi linalopinga kuongezwa kwa viwaqnda vya kuzalisha mafuta alijifunga kwenye mhimili wa lango na kuzua mtafaruku uwanjani Goodson Park.

Image: GOAL

Mechi ya ligi kuu ya Premia nchini Uingereza kati ya Everton na Newcastle ilisitishwa kwa muda baada ya shabiki mmoja mwandamanaji kujifunga kwenye mhimili wa goli kunako dakika ya 49 kipindi cha pili.

Mechi ilisitishwa kwa zaidi ya dakika tano ambapo walinzi waliingia, wakamfungua na kumsindikiza nje ya uwanja. Shabiki huyo alikuwa amevalia shati ya rangi ya machungwa yenye maandishi 'Just Stop Oil'

Kundi la kampeni la "Just Stop Oil" limedai kuhusika na msukosuko huo. Waliandika kwenye Twitter: "Mfuasi wa Just Stop Oil alijifunga kwa goli wakati wa mechi ya Everton dhidi ya Newcastle United."

Kundi hilo liliongeza: "Jioni ya leo, Louis, mwenye umri wa miaka 21, mfuasi wa Just Stop Oil, alijifungia kwenye goli kwenye uwanja wa Goodison Park akiwa amevalia t-shirt ya Just Stop Oil, na kusababisha mwamuzi kusitisha mchezo kwa muda."

Kundi hilo la kiharakati linaandamana kupinga hatua ya serikali ya Uingereza kuendelea kufungua viwanda vya kuzalisha mafuta katika maeneno ya North Sea ambapo wanasema hatua hiyo inahatarisha usalama wa mustakabali wa watoto wao kwani inachafua mazingira.

Kulingana na taarifa kwenye mitandao ya kundi hilo, wanadai “Ikiwa tutapoteza udhibiti wa hali ya hewa yetu, ambayo ndiyo hasa tunakoelekea kwa sasa, basi tunaweka kila kitu na kila mtu hatarini. Kizazi changu hakitakuwa na wakati ujao.”