Fahamu kwa nini Kombe la Dunia kufanyika Qatar kumezua utata

Muhtasari

•Kuna maswali kuhusu jinsi Qatar ilishinda haki ya kuhodhi michuano hiyo, jinsi inavyowashughulikia wafanyakazi wanaojenga viwanja vya michezo, na kama ni eneo linalofaa kwa michuano hiyo.

Image: GETTY IMAGES

Droo ya fainali za Kombe la Dunia za kandanda za mwaka huu - katika taifa la Mashariki ya Kati la Qatar - itafanyika Ijumaa Aprili 1.

Ni Kombe la Dunia lenye utata kuwahi kutokea, huku kukiwa na maswali kuhusu jinsi Qatar ilishinda haki ya kuhodhi michuano hiyo, jinsi inavyowashughulikia wafanyakazi wanaojenga viwanja vya michezo, na kama ni eneo linalofaa kwa michuano hiyo.

Walivyotendewa wafanyakazi wa kigeni

Qatar inajenga viwanja saba kwa ajili ya fainali hizo, uwanja wa ndege mpya, metro na barabara mpya.

Fainali hiyo itachezwa katika uwanja ambao pia unachezwa mechi nyingine tisa, ambao ni kitovu cha jiji jipya.

Lakini serikali imesababisha kuwepo kwa ukosoaji kwa matendo yake kwa wafanyakazi wa kigeni 30,000 wanaofanya kazi kwenye miradi hiyo.

Mnamo mwaka 2016, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilishutumu Qatar kwa kutumia mabavu dhidi ya wafanyakazi. Ilisema wafanyiaazi wengi walikuwa wakiishi katika makazi duni, wakilipa ada kubwa za kuajiri na wamezuiliwa mishahara na kunyang'anywa hati za kusafiria.

Image: GETTY IMAGES

Tangu mwaka 2017, serikali ilianzisha hatua za kuwalinda vibarua wahamiaji wasifanye kazi kwenye joto jingi, kupunguza saa zao za kazi na kuboresha hali zao katika kambi za wafanyakazi.

Hata hivyo, kikundi cha kampeni cha Human Rights Watch kilisema katika ripoti ya mwaka 2021 kwamba wafanyakazi wa kigeni bado wanateseka kutokana na "kukatwa kwa mishahara ya adhabu na kinyume cha sheria", pamoja na "miezi ya mishahara isiyolipwa kwa saa nyingi za kazi ngumu".

Amnesty International pia imesema kuwa pamoja na kukomeshwa kwa mfumo wa "kafala" - au ufadhili - ambao uliwazuia wafanyakazi wahamiaji kuacha kazi zao bila ridhaa ya mwajiri wao, shinikizo bado lilikuwa likiwekwa kwa wafanyakazi.

Image: GETTY IMAGES

Msemaji wa serikali aliiambia BBC: "Maendeleo makubwa ya kuhakikisha mageuzi yanatekelezwa ipasavyo yamepatikana." Ilisema idadi ya kampuni zinazovunja sheria "itaendelea kupungua kadiri hatua za utekelezaji zinavyoendelea".

Wafanyakazi wangapi walipoteza maisha?

Mnamo Februari 2021, gazeti la Guardian lilisema wafanyakazi wahamiaji 6,500 kutoka India, Pakistan, Nepal, Bangladesh na Sri Lanka walikufa huko Qatar tangu iliposhinda zabuni yake ya kuhodhi michuano ya Kombe la Dunia.

Vifo hivyo, ambavyo viliripotiwa na mamlaka katika nchi tano za Asia, havikuwekwa kulingana na kazi au mahali. Lakini shirika la kutetea haki za wafanyakazi la FairSquare lilisema kuna uwezekano kwamba wengi wa wale waliokufa walikuwa wakifanya kazi katika miradi ya miundombinu.

Serikali ya Qatar inasema takwimu hizo ni za kupita kiasi, kwa sababu zinajumuisha maelfu ya wageni waliofariki baada ya kuishi na kufanya kazi huko kwa miaka mingi. Inasema wengi wangekuwa wakifanya kazi zisizohusiana na tasnia ya ujenzi.

Qatar inasema kuwa kati ya 2014 na 2020, kulikuwa na vifo 37 kati ya wafanyakazi waliojenga viwanja vya Kombe la Dunia. Inasema 34 kati ya hizo hazikuwa "zinazohusiana na kazi".

Image: GETTY IMAGES

Shirika la Kazi Duniani (ILO) linasema Qatar haijahesabu vifo vya ghafla na visivyotarajiwa miongoni mwa vibarua. Inasema haya ni pamoja na mshtuko mbaya wa moyo na kushindwa kupumua kunakosababishwa na joto kali kilichorekodiwa kuwa kutokana na "sababu za asili" badala ya "kuhusiana na kazi".

ILO imekusanya takwimu zake za vifo kutoka hospitali zinazosimamiwa na serikali na huduma za magari ya kubeba wagonjwa nchini Qatar, zinazoshughulikia majeruhi kutoka kwa miradi yote inayohusiana na Kombe la Dunia.

Inasema wafanyakazi 50 walikufa na wengine zaidi ya 500 walijeruhiwa vibaya nchini Qatar mnamo 2021 pekee, na wengine 37,600 walipata majeraha madogo hadi ya wastani.

Sababu kuu za vifo na majeraha haya ni kuanguka kutoka maeneo yenye urefu, ajali za barabarani na kuanguka kwa vitu.

Je, Qatar ilipataje nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia?

Qatar 2022 imekuwa na utata tangu ilipotangazwa na shirikisho la soka duniani Fifa mwaka 2010.

Ikiwa ni nchi ndogo sana (kama tajiri sana) yenye historia ndogo ya soka, na halina rekodi ya kuwahi kufuzu kwa Kombe la Dunia, ilishangaza wengi wakati Qatar iliposhinda ushindani dhidi ya Marekani, Australia, Korea Kusini na Japan.

Uamuzi huo uliibua madai kuwa maafisa wa Fifa walikuwa wamehongwa ili kuipa nafasi hiyo Qatar, ingawa uchunguzi huru ulioamriwa na Fifa baadaye haukupata ushahidi mzito wa hili.

Qatar inakanusha madai kwamba ilinunua kura za wajumbe, lakini uchunguzi wa rushwa na mamlaka ya Ufaransa bado unaendelea, na mwaka 2020 Marekani ilishutumu maafisa watatu wa Fifa kwa kupokea hongo.

Image: GETTY IMAGES

Kwa nini Kombe la Dunia la Qatar litafanyika msimu wa baridi?

Mashindano ya Kombe la Dunia kwa kawaida hufanyika Juni na Julai, lakini nchini Qatar wastani wa halijoto wakati huo wa mwaka ni takriban 41C (106F) na inaweza kufikia 50C (122F) - joto sana kuwa nje na ukawa salama, achilia mbali kucheza takribani dakika 90.

Wakati wa mchakato wa zabuni, Qatar iliahidi teknolojia ya hali ya juu ya viyoyozi ambayo ingepoza viwanja, viwanja vya mazoezi na maeneo ya mashabiki hadi 23C. Hata hivyo, mwaka 2015 uamuzi ulitolewa na Fifa kuandaa michuano hiyo wakati wa baridi.

Kombe la Dunia litaanza Novemba 21, na fainali ni tarehe 18 Desemba. Hii ina maana iko katikati na kuvuruga msimu wa soka wa klabu kwa nchi nyingi.

Ligi Kuu ya Uingereza, kwa mfano, haitashuhudia mechi yoyote itakayochezwa kati ya Novemba 13 na 26 Desemba.

Ili kufidia muda uliopotea, msimu wa 2022/2023 utaanza wiki moja mapema kuliko kawaida na kumalizika wiki moja baadaye.