Msemaji wa Yanga hatambui uzalendo, aikaribisha Orlando Pirates kupiga Simba SC katika CAFCC

Muhtasari

• “Wananchi wenzenu mtatukuta huku huku. Njooni wanaume Orlando Pirates vivaaaaa,” aliandika Haji Manara kwenye post hiyo ya Orlando.

Msemaji wa klabu ya Yanga, Haji Sunday Manara
Msemaji wa klabu ya Yanga, Haji Sunday Manara
Image: Instagram

Msemaji wa klabu cha soka cha Yanga kutokea Tanzania ameshangaza wengi baada ya kusema kwamba mashabiki wa timu hiyo hawatoweka uzalendo mbele na kuishabikia timu ya Simba ambao ni mahasimu wao tangu jadi katika mchuano wa robo fainali ya kombe la mashirikisho CAF utakaowakutanisha dhidi ya Orlando Pirates ya jamhuri ya Afrika Kusini.

Manara aliandika kwenye ukurasa wa miamba hao kutoka Afrika Kusini kwa kuwaambia kwamba mashabiki wa Yanga wataishabikia pindi tu wakatapotua nchini Tanzania kucheza dhidi ya Simba.

“Safari ya Tanzania inatusubiria,” waliandika Orlando Pirates kwenye Instagram yao.

“Wananchi wenzenu mtatukuta huku huku. Njooni wanaume Orlando Pirates vivaaaaa,” aliandika Haji Manara kwenye post hiyo ya Orlando.

Wengi walikuwa wanategemea kwamba timu mbali mbali zitaweka upinzani wao kando na kujibwaga nyuma ya timu ya Simba ambayo kinadharia inawakilisha taifa zima katika michuano ya CAF lakini kwa Manara, bado bato lipo pale pale.

Msemaji huyo mwenye uzoefu mkubwa alikuwa zamani msemaji wa Simba kabla ya kutofautiana kimkataba na kikazi ambapo msimu huu aligeuza kadi na kuingia Yanga, timu ambayo alikuwa anaichamba pakubwa kwa jina Utopolo.