(VIDEO) Ronaldo aomba msamaha kwa kuvunja simu ya shabiki, aahidi kumfadhili kutazama mechi Old Trafford

Muhtasari

• CR7 - Ningependa kuomba radhi kwa mlipuko wangu na, ikiwezekana, ningependa kumwalika shabiki yule kutazama mchezo huko Old Trafford.

Mchezaji wa Man-U, Christiano Ronaldo
Mchezaji wa Man-U, Christiano Ronaldo
Image: Facebook

Siku ya Jumamosi kioja kilishuhudiwa katika uga wa nyumbani wa timu ya Everton, Goodson Park katika mechi ya ligi kuu ya Uingereza kati ya timu hiyo na Manchester United, ambapo mshambuliaji wa United nguli Christiano Ronaldo kwa ghadhabu alipasua simu ya shabiki aliyetaka kupiga picha naye.

Ronaldo aliyejawa na hasira mithili ya mkizi kutokana na timu yake kupoteza kwa kufungwa bao moja kwa nunge na Everton ambayo inashikilia nafasi ya nne kuelekea mkiani, alimsukuma na kuipasua simu ya shabiki huyo wa Everton aliyejawa na furaha baada ya kumuona mchezaji huyo maarufu duniani na kutaka kuchukua picha na yeye.

Baada ya kukashifiwa pakubwa kwa kitendo hicho, hatimaye mchezaji huyo alilazimika kuomba msamaha kwa shabiki huyo mchanga na kusema kwamba si kupenda kwake kwa tukio lile bali ni kutokana na kukwazika kwa kupoteza mechi muhimu ambayo ingeihakikishia timu yake nafasi ya kuingia nne bora ili kufuzu mechi za klabu bingwa barani Ulaya msimu kesho.

Pia alisema kama inawezekana shabiki huyo kumsamehe basi atamualika kwa gharama yake kuhudhuria mechi katika uga wa Old Trafford, uwanja wa nyumbani wa Manchester United.

“Si rahisi kamwe kushughulika na hisia katika nyakati ngumu kama vile tunazokabiliana nazo. Hata hivyo, daima tunapaswa kuwa na heshima, subira na kuweka mfano kwa vijana wote wanaopenda mchezo huo mzuri. Ningependa kuomba radhi kwa mlipuko wangu na, ikiwezekana, ningependa kumwalika shabiki yule kutazama mchezo huko Old Trafford kama ishara ya mchezo wa haki na kwa moyo wa kimichezo,” aliandika Ronaldo kwenye mitandao yake ya kijamii.

Msamaha wake ulikuja pindi tu taarifa zilipozuka kwamba polisi katika mji wa Merseyside huko Uingereza wameanzisha uchunguzi dhidi ya Ronaldo kwa tukio hilo la kukosa nidhamu kwa kupasua simu ya shabiki mchanga ambaye kosa lake ni kutaka picha na yeye.