(VIDEO)"Ubatizo wa moto au uchawi?" Mashabiki watania matibabu ya taulo moto kwa Michael Olunga

Muhtasari

• "Huu ni uchawi" mashabiki wamjia juu mshambuliaji Michael Olunga kwa video ya matibabu kutumia taulo moto.

Mchezaji Michael Olunga akipokea matibabu ya moto
Mchezaji Michael Olunga akipokea matibabu ya moto
Image: Facebook///Michael Olunga

Mashabiki wa kandanda nchini Kenya wamefurika katika mtandao wa Facebook wa mchezaji wa kimataifa Michael Olunga wakitaka kujua maana ya video ambayo alipakia pale akikandwa mgongoni na taulo lenye moto.

Olunga alipakia video hiyo akisema kwamba ni njia moja ya kuhudumiwa kama matibabu ili kujiandaa kwa msimu unaokuja wa mchezo wa kandanda katika ligi kuu ya Qatar.

Mshambuliaji huyo wa timu ya Al Duhail alipakia video hiyo inayomuonesha akiwa amelala kifudifudi huku mwanaume mmoja akiwa anamkanda mgongoni kwa taulo hilo linaloonekana kutoka moto kabisa.

“Wale mnaojua hii recovery inaitwaje? Mlisema hii ndio photo moto?” aliandika Olunga baada ya mashabiki wengi kuonekana kuchanganyikiwa.

Wengi walisiojua njia hiyo ya kutomaswa na kukandwa walihisi kabisa mchezaji huyo ameenda kutafuta huduma za kishirikina kwa waganga na wachawi wa uarabuni.

“Olunga tafadhali unaweza kueleza ni aina gani ya matibabu hayo sasa kabla tuhitimishe ni uchawi uharabuni,” aliandika Fidelian Jose, mmoja wa mashabiki wake.

“Mambo kama haya yakifanywa Afrika, basi yanaitwa uchawi, lakini kwa sababu ni kwa watu wasio Weusi basi yanaitwa matibabu,” mwingine alitania.