Meneja Mikel Arteta aongeza mkataba wake na Wanabunduki

Muhtasari

•Arteta ametia saini mkataba mpya wa miaka miwili ambao utamuweka Emirates hadi mwisho wa msimu wa 2024/25.

•Mmoja wa wamiliki wa klabu hiyo Josh Kroenke amesema ni furaha yao kuongeza kandarasi za Arteta na Eidvall.

Image: WWW.ARSENAL.COM

Klabu ya Arsenal imewakabidhi makocha wake wawili Mikel Arteta na Jonas Eidvall kandarasi mpya.

Arteta ambaye ndiye meneja wa klabu hiyo ametia saini mkataba mpya wa miaka miwili ambao utamuweka Emirates hadi mwisho wa msimu wa 2024/25.

"Nimefurahia, ninashukuru na kwa kweli nina furaha sana leo," Arteta alisema baada ya kutia saini mkataba huo.

Raia huyo wa Uhispania amesema lengo lake ni kupeleka Arsenal katika hadhi ya juu zaidi na kuiweka katika nafasi ya kupimana nguvu na vilabu vingine vikubwa.

"Ili kufanya hivyo, lazima tucheze Ligi ya Mabingwa. Tunapaswa kuwa na uwezo wa kuendeleza timu, kuboresha wachezaji wetu, kuboresha idara zote, kuzalisha uhusiano zaidi na mashabiki wetu, kuboresha hali ya Emirates, kuwa na uwezo wa kuajiri vipaji vya juu zaidi  na watu bora kwa klabu hii kuendesha  mradi huu kufikia hatua hiyo," Alisema Arteta.

Jonas Eidevall ambaye ni kocha wa timu ya wanabunduki ya wanawake ametia saini mkataba wa mwaka mmoja.

Eidvall ambaye amekuwa na msimu mzuri na timu hiyo amesema ataendelea kutoa huduma zake "kwa klabu niipendayo na kuwa na watu ninaowapenda."

Mmoja wa wamiliki wa klabu hiyo Josh Kroenke amesema ni furaha yao kuongeza kandarasi za wakufunzi hao wawili.

Arteta alijiunga na Wanabunduki mwaka wa 2019 na msimu huu ameweza kufufua ndoto za klabu hiyo kucheza katika Champions League.