Rasmi! Mshambuliaji Erling Haaland kujiunga na Manchester City

Muhtasari

•Jumanne jioni mabingwa hao wa EPL mara tano walitanganza kuwa Halaand atakuwa anajiunga nao rasmi mnamo Julai 1, 2022.

•Manchester City imetangaza kuwa makubaliano ya masharti kati ya klabu na Halaand bado yanaendelea.

Washambulizi Erling Haaland na Phil Foden
Washambulizi Erling Haaland na Phil Foden
Image: EPL

Klabu ya Manchester City imeafikia makubaliano na Borussia Dortmund kwa uhamisho wa mshambuliaji matata Erling Halaand.

Jumanne jioni mabingwa hao wa EPL mara tano walitanganza kuwa Halaand atakuwa anajiunga nao rasmi mnamo Julai 1, 2022.

"Manchester City inaweza kuthibitisha kwamba tumefikia makubaliano kimsingi na Borrusia Dortmund kwa uhamisho wa mshambuliaji Erling Halaand kujiunga na klabu tarehe 1 Julai 2022," City ilitangaza kupitia tovuti rasmi ya klabu.

Mabingwa hao watetezi wa ligi ya Premier wametangaza kuwa makubaliano ya masharti kati ya klabu na Halaand bado yanaendelea.

City inatarajiwa kulipa Dortmund ada isiyopungukia Euro milioni 60. Haaland atakuwa miongoni mwa wachezaji wanaopokea mshahara mkubwa zaidi huku akilipwa takriban pauni 375, 000 kwa wiki.

Premier League imemkaribisha mzaliwa huyo wa Norway ambaye tayari ameonyesha umahiri mkubwa wa soka licha ya kuwa na miaka 21 tu.

Kufikia sasa Haaland ndiye mfungaji bora wa tatu katika Bundesliga huku akiwa amefunga mabao 21 na kusaidia katika mabao 7.

Mshambulizi huyo ndiye mfungaji bora wa Dortmund tangu alipojiunga nao takriban miaka miwili iliyopita.