Tazama jinsi EPL 2021/22 ilivyotamatika

Muhtasari

•City ilishinda taji la EPL 2021/22 kwa pointi 93, alama moja tu juu ya Liverpool ambayo ilizoa pointi 92.

•Msimu wa EPL 2022/23 unatarajiwa kung'oa nanga mnamo Agosti 6, 2022 na ukamilike Mei 28, 2023.

Image: PREMIER LEAGUE

Msimu wa 2021/22 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ulifika hatima Jumapili jioni huku Manchester City ikinyakua taji hilo.

Jumla ya mechi 10 zilichezwa katika viwanja mbalimbali nchini Uingereza mnamo siku ya mwisho ya ligi.

Vijana wa Pep Guardiola walisubiri mpaka dakika ya mwisho ya mechi yao dhidi ya Aston Villa iliyochezwa ugani Etihad ili kuthibitisha uongozi wao katika jedwali. Dalili za kombe hilo kuwaponyoka zilikuwa zimeanza kuonekana katika dakika za mwisho baada ya Villa kuchukua uongozi wa 0-2 katika dakika za kwanza 75.

Hata hivyo mshambulizi Iikay Gundogana na kiungo Rodri walinusuru klabu yao kwa kufunga mabao mawali na moja mtawalia kabla ya kipenga kupulizwa.

City ilishinda taji la EPL 2021/22 kwa pointi 93, alama moja tu juu ya Liverpool ambayo ilizoa pointi 92.

Katika mechi ya mwisho, Liverpool iliandikisha ushindi wa 3-1 dhidi ya Wolves ambao walichukua nafasi ya 10 kwenye jedwali kwa pointi 51.

Chelsea na Tottenham walijinyakulia nafasi katika Champions League msimu ujao baada ya kuandikisha ushindi katika mechi za mwisho.

Chelsea iliandikisha ushindi wa 2-1 nyumbani dhidi ya Watford ambao tayari walikuwa wameshushwa daraja.

Tottenham waliwika ugenini dhidi ya Norwich kwa kuwachapa mabao tano kwa mtungi. Norwich pia walikuwa wameshushwa daraja.

Wanabunduki walikosa nafasi katika Champions League licha ya kupata ushindi mkubwa wa 5-1 dhidi ya Everton katika mechi iliyochezewa ugani Emirates.

Arsenal na Manchester United sasa watashiriki  katika Europa League msimu ujao baada ya kuchukua nafasi ya 5 na 6 mtawalia kwa pointi 69 na 58.

United walipoteza 1-0 katika mechi ya mwisho ugenini dhidi ya Crystal Palace.

Nafasi ya saba ilichukuliwa na West Ham ambao walipoteza 1-3 dhidi ya Brighton katika mechi ya mwisho.

Leicester na Brighton walichukua nafasi za 8 na 9 mtawalia wakimaliza na  pointi 52 na 51.

Burnley, Watford na Norwich zilishiriki katika Championship msimu ujao baada ya kuchukua nafasi za 18, 19 na 20 mtawalia.

Nafasi za timu hizo tatu zilizoshushwa daraja zitachukuliwa na Fulham, Bournemouth na moja kati ya Huddersfield, Nottingham Forest, Sheffield United ama Luton msimu ujao.

Msimu wa EPL 2022/23 unatarajiwa kung'oa nanga mnamo Agosti 6, 2022 na ukamilike Mei 28, 2023.