Rasmi! Uuzaji wa klabu ya Chelsea kwa kampuni ya Marekani wakamilika

Muhtasari

•Chelsea imekuwa ikifanya operesheni zake chini ya leseni maalum ya serikali ambayo ilitarajiwa kuisha tarehe 31 mwezi Mei.

Todd Boehly
Todd Boehly
Image: BBC

Uuzaji wa klabu ya Chelsea wa £4.25bn kwa kampuni inayoongozwa na muwekezaji wa Marekani Todd Boehly pamoja na kampuni ya kibinafsi ya Clearlake Capital umekamilika

Klabu hiyo ilianza kuuzwa mwezi Machi kabla ya mmiliki wake wa zamani Roman Abramovich kuwekewa vikwazo kutokana na uhusiano wake na rais wa Urusi Vladimir Putin.

Chelsea imekuwa ikifanya operesheni zake chini ya leseni maalum ya serikali ambayo ilitarajiwa kuisha tarehe 31 mwezi Mei.

Boehly alisema alifurahia hatua hiyo na alitaka kuwafanya mashabiki wa klabu hiyo kujivunia. Kampuni hiyo ilikabiliana na wapinzani 11 kuwa mmiliki mpya wa klabu hiyo , katika mchakato wa mauzo ulioanza tarehe 2 Machina ulikuwa na zaidi ya maombi 250 ya wanunuzi.

‘’Tunafurahia kuwa wamiliki wapya wa klabu ya Chelsea’’ , alisema.

‘’Tuko asilimia 100 kila dakika ya kila mechi. Lengo letu kama wamiliki liko wazi . Tunataka kuwafanya mashabiki wajivunie’’.

‘Pamoja na kujitolea kwetu na kuendeleza soka ya vijana ili kujipatia talanta bora , mpango wetu ni kuwekeza katika klabu kwa muda mrefu na kujenga historia nzuri ya Chelsea’.

‘Mimi binafsi nataka kuwashukuru mawazirina maafisa katika serikali ya Uingerezana ligi ya premia , kwa kuhakikisha kuwa hili linafanikiwa’.

Serikali ya Uingereza – ambayo ilisema Jumatano ijayo, itatoa leseni kwa lengo la kuiuza klabu hiyo – haitaki Abrahamovich apate faida yoyote kutoka kwa mauzo hayo , ambazo badala yake zitaelekea katika akaunti zilizopigwa tanji ili kusaidia mashirika ya hisani yanayowasaidia waathiriwa wa vita vya Ukraine.