Kylian Mbappe: Mshambulizi wa Paris St-Germain aorodheshwa kuwa mchezaji wa thamani zaidi duniani

Muhtasari

• Mshambulizi huyo wa Ufaransa Mbappe alisaini mkataba mpya wa miaka mitatu na PSG mwezi uliopita.

 

Mshindi wa Kombe la Dunia Kylian Mbappe ameorodheshwa kama mchezaji wa thamani zaidi duniani, mbele ya Vinicius Jr na Erling Haaland.
Mshindi wa Kombe la Dunia Kylian Mbappe ameorodheshwa kama mchezaji wa thamani zaidi duniani, mbele ya Vinicius Jr na Erling Haaland.
Image: GETTY IMAGES

Kylian Mbappe, Vinicius Jr na Erling Haaland ndio wachezaji wa thamani zaidi ulimwenguni, kulingana na utafiti wa kikundi cha CIES Football Observatory.

Mbappe, 23, ambaye alikataa kuhamia Real Madrid na kusalia Paris St-German, anaongoza orodha hiyo akiwa na thamani ya uhamisho wa euro milioni 205.6 au pauni milioni 175.7.

Winga wa Real Madrid Mbrazil Vinicius Jr, ambaye alifunga bao la ushindi katika fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Liverpool, anashika nafasi ya pili akiwa kwa pauni milioni 158.3, huku mshambuliaji wa Norway anayekwenda Manchester City, Haaland akiwa wa tatu kwa pauni milioni 130.4m.

Kiungo wa kati wa Borussia Dortmund Jude Bellingham, pauni milioni 114.1, ndiye mchezaji wa Uingereza mwenye thamani kubwa zaidi kwenye orodha hiyo katika nafasi ya tano, mbele ya mchezaji mwenza wa timu ya Uingereza na kiungo wa kati wa Manchester City Phil Foden katika nafasi ya sita kwa pauni milioni 105.9.

Vilabu vya Premier League vinatawala orodha hiyo na wawakilishi 41 katika 100 bora.

CIES hutumia mambo tofauti ikiwa ni pamoja na umri wa mchezaji, uchezaji, thamani ya kiuchumi ya klabu yao na mfumuko wa bei ili kutathmini makadirio ya thamani za uhamisho.

Mshambulizi wa Ufaransa Mbappe alisaini mkataba mpya wa miaka mitatu na PSG mwezi uliopita huku akichagua kusalia Paris badala ya kuhamia kwa mabingwa wa La Liga na Ligi ya Mabingwa, Real Madrid.

Mshindi huyo wa Kombe la Dunia alifunga mabao 28 kwenye Ligue 1 na kuisaidia PSG kushinda taji la mwaka 2021-22.

Haaland, 21, anajiunga na Manchester City kutoka Borussia Dortmund baada ya City kuamsha kipengele chake cha uhamisho cha euro milioni 60 (pauni milioni 51.2). Mchezaji mwenzake mpya wa City Ruben Dias ndiye beki mwenye thamani zaidi katika nafasi ya tisa kwa pauni milioni 93.6.

Mchezaji bora wa Ligi ya Premia msimu huu, Kevin de Bruyne mwenye umri wa miaka 30 wa Manchester City, ndiye mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi katika 100 bora ( pauni milioni 48.9) na Gavi mwenye umri wa miaka 17 wa Barcelona ( pauni milioni 49.9) ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi.

Wakati huohuo, Gianluigi Donnarumma wa PSG, ambaye alishinda Ubingwa wa Ulaya akiwa na Italia, ndiye kipa mwenye thamani kubwa zaidi akiwa katika nafasi ya 41 kwenye viwango vya ubora (pauni milioni 62.9).

Washindi wa pili wa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa msimu huu, Liverpool, wanawakilishwa katika 10 bora na usajili wa Januari wa Luis Diaz ( pauni milioni 94).

Wachezaji watatu wa Barcelona Pedri, Frenkie de Jong, ambaye amekuwa akihusishwa na Manchester United, na Ferran Torres wote wamejumuishwa katika 10 bora.

Wachezaji wa kimataifa wa Uingereza, Jadon Sancho (£88.1m), Mason Mount (pauni milioni 85.7) na Bukayo Saka (pauni milioni 85.6) wako nafasi ya 13, 14 na 15 mtawalia.

Darwin Nunez, ambaye amekuwa akihusishwa pakubwa na kuhama kutoka Benfica, ana thamani ya juu zaidi ( pauni milioni 59.9) kwa wachezaji nje ya ligi tano bora za Ulaya.