Yote unayopaswa kufahamu kuhusu Kombe la Dunia Qatar

Muhtasari

•Michuano hiyo itakayoanza mwezi Novemba, itakuwa ni Kombe la Dunia la kwanza kufanyika Mashariki ya Kati na la kwanza wakati huu wa mwaka.

•Waandalizi wa Kombe la Dunia wamejibu kuwa "kila mtu anakaribishwa", lakini Qatar haitalegeza sheria zake kuhusu ushoga.

Image: BBC

Nafasi mbili za mwisho katika fainali za Kombe la Dunia za 2022 zitaamuliwa wiki hii wakati mechi za mchujo za mabara zitafanyika huko Doha, Qatar.

Michuano hiyo itakayoanza mwezi Novemba, itakuwa ni Kombe la Dunia la kwanza kufanyika Mashariki ya Kati na la kwanza wakati huu wa mwaka. Hata hivyo, uamuzi wa kufanyika nchini Qatar umezua utata.

Ni lini Kombe la Dunia la 2022 litafanyika na litakuwa moto kiasi gani?

Fainali za Kombe la Dunia zinafanyika kati ya Novemba 21 na 18 Desemba - wakati ambapo hali ya joto nchini Qatar kawaida hufikia nyuzi joto 25C (77F).

Kama fainali zingefanyika Juni na Julai, kama kawaida, mechi zingechezwa kwenye joto linalozidi 40C na wakati mwingine kufikia 50C.

Awali Qatar ilipendekeza kufanyika kwa fainali hizo wakati wa majira ya kiangazi katika viwanja vilivyokuwa na viyoyozi, lakini mpango huo ulikataliwa.

Image: BBC

Je, kuna matatizo gani katika kuandaa Kombe la Dunia wakati wa baridi?

Novemba na Desemba ni miezi yenye shughuli nyingi kwa vilabu vya soka vya Ulaya na wachezaji wengi wataitwa kuchezea nchi zao huko Qatar 2022.

Kwa hivyo, ligi za Ulaya kama vile Ligi Kuu ya England, Serie A ya Italia na La Liga ya Hispania zitalazimika kusimam kwa wiki moja kabla ya kuanza kwa kombe la dunia. Watazianzisha upya baada ya kumalizika kwa fainali hizo.

Kwa nini Qatar ilichaguliwa kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia?

Mnamo 2010, Qatar ilinyakua haki za Kombe la Dunia kwa kushinda kura ya wajumbe 22 wakuu wa Fifa. Ilishinda zabuni kutoka Marekani, Korea Kusini, Japan na Australia.

Ni taifa la kwanza la Kiarabu kuandaa michuano hiyo.

Qatar ilishutumiwa kwa kuwalipa maafisa wa Fifa pauni milioni 3 ($3.7m) kama hongo ili kupata uungwaji mkono wao lakini iliondolewa baada ya uchunguzi wa miaka miwili.

Mwenyekiti wa wakati huo wa Fifa, Sepp Blatter, aliunga mkono ombi la Qatar wakati huo, lakini tangu wakati huo amesema Fifa huenda ilifanya uamuzi usio sahihi.

Kwa sasa Bw Blatter anashtakiwa nchini Uswizi kwa makosa ya ulaghai, ubadhirifu na mashtaka mengine ya ufisadi.

Image: BBC

Qatar pia imekabiliwa na madai ya Amnesty International na Human Rights Watch ya kukukiuka haki za binadamu kwa kuwatendea vibaya wafanyakazi wa kigeni ambao wamekuwa wakijenga viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya Kombe la Dunia.

Je, ni timu gani zilizofuzu Kombe la Dunia na ni nani anayepewa kipaumbele zaidi?

Hatua za kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2022 zilianza miaka mitatu iliyopita.

Timu kutoka mabara tofauti zilicheza katika hatua ya makundi, na timu za juu zilifuzu kwenda fainali, huku nyingine zikifuzu kupitia mchujo.

Ufaransa, washindi wa Kombe la Dunia la 2018, walifanikiwa lakini mabingwa wa sasa wa Ulaya Italia walishindwa kufuzu.

Katika fainali hizi, timu 32 zilipangwa katika makundi nane ya timu nne nne. Timu kutoka bara moja zilitengwa - isipokuwa kwa nchi za Ulaya, ambapo timu mbili za juu zinaweza kuwa katika kundi lolote.

Brazil, England, Ufaransa na Hispania ndio wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda kombe hilo mwaka huu.

Qatar, ambayo ina wakazi milioni 2.9, ni mojawapo ya nchi tajiri zaidi duniani kutokana na mauzo yake ya mafuta na gesi. Imejenga viwanja saba mahsusi kwa ajili ya mashindano hayo, na jiji zima ambalo litaandaa mechi ya fainali.

Zaidi ya hoteli 100 mpya, treni mpya, barabara mpya pia zinajengwa.

Kamati ya maandalizi ya michuano hiyo inakadiria kuwa watu milioni 1.5 watahudhuria fainali hizo.

Qatar ni nchi ya Kiislamu ya kihafidhina, na mashabiki wameonywa kuwa waangalifu kuhusu tabia zao,

Kuna vikwazo vikali vya kunywa pombe. Kawaida pombe inaweza kununuliwa tu katika baa za hoteli za kifahari. Gharama ya bia moja inagharimu hadi dola $13.

Hata hivyo, waandalizi wanasema pombe huenda ikauzwa katika maeneo maalum ya mashabiki wakati wa fainali hizo.

Nini rekodi ya Qatar kuhusu haki za mashoga?

Vitendo vya ushoga ni haramu nchini Qatar.

Makundi yanayowakilisha mashabiki wa soka ya mashoga yamekuwa yakiiomba serikali yake "kuhakikisha usalama wao", huku baadhi ya mashabiki wa Wales wakisema watasusia mashindano hayo kufuatia kufuzu kwa timu yao.

Waandalizi wa Kombe la Dunia wamejibu kuwa "kila mtu anakaribishwa", lakini Qatar haitalegeza sheria zake kuhusu ushoga.