Real Madrid yamkaribisha Antonio Rudiger kutoka Chelsea

Muhtasari

•Klabu ya Laliga inayoongozwa na Carlo Ancelotti ilitangaza kuwa beki huyo alifuzu vipimo vyake vya afya kama ilivyohitajika.

•Rudiger alipongeza mafanikio ya awali ya klabu hiyo huku akibainisha kuwa lengo lake  kuu ni kushinda mataji pale.

Antonio Rudiger amejiunga rasmi na Real Madrid
Antonio Rudiger amejiunga rasmi na Real Madrid
Image: REAL MADRID

Beki wa timu ya taifa ya Ujerumani Antonio Rudiger amejiunga rasmi na klabu ya Real Madrid kutoka Chelsea.

Klabu hiyo ya Uhispania ilitangaza kujiunga kwa Rudiger siku ya Jumatatu kupitia kurasa zao rasmi  za mitandao ya kijamii.

"Tumeimarisha kikosi chetu kwa kumsajili mmoja wa mabeki bora katika soka la dunia baada ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani kujiunga na klabu hiyo akitokea Chelsea," Real Madrid ilitangaza kupitia tovuti yake rasmi.

Klabu ya Laliga inayoongozwa na Carlo Ancelotti ilitangaza kuwa beki huyo alifuzu vipimo vyake vya afya kama ilivyohitajika. 

Rudiger alipongeza mafanikio ya awali ya klabu hiyo huku akibainisha kuwa lengo lake  kuu ni kushinda mataji pale.

"Real Madrid ina wachezaji wengi wa hadhi ya juu, haswa katika nafasi yangu, lakini ninajiamini sana. Mchango wangu utatokana na makali ya ushindani, kipengele cha afya kwa wakati wowote na kitu ambacho kinatusukuma kuendelea kupigana. Ni changamoto ambayo iliibua shauku yangu,” Rudiger alisema katika hotuba yake baada ya kujiunga na klabu hiyo.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 29 alikamilisha uhamisho wake kutoka Chelsea mapema mwezi Juni.

Rudiger alijiunga na Real Madrid bila ada yoyote kwani mkataba wake na Chelsea ulikuwa unaelekea kuisha.

"Rudiger ameondoka The Blues na kujiunga na Real Madrid, akiwa ametoa mchango mkubwa katika mafanikio yetu katika misimu ya hivi karibuni. Rudiger alinyanyua Kombe la FA, Ligi ya Mabingwa, Ligi ya Europa, UEFA Super Cup na Kombe la Dunia la Vilabu la FIFA akiwa na Chelsea huku akicheza jukumu muhimu katika ushindi huo wote katika moyo wa ulinzi wetu,"  Chelsea ilitangaza kupitia taarifa.

Beki huyo ambaye alijiunga na Chelsea mwaka wa 2017 aliondoka baada ya kuwakilisha klabu hiyo katika mechi 203 na kuifungia jumla ya mabao 12