"Niliipenda Simba SC sana, lakini wamenikatisha tamaa" - Benard Morrison

Masaibu yake na klabu ya Simba yalianza pale alipofurushwa mazoezini kwa utovu wa nidhani na baadae kutakiwa kuchukua likizo ya lazima kutoka timuni

Muhtasari

• “CEO aliniita ofisini kwake akaniambia wachezaji wengine hawanitaki kwa hiyo nikae mbali na timu" - Morrison.

• Mchezaji huyo aliwataka mashabiki wampe jezi 100 kuwagawia watu kwao Ghana kama njia ya kuonesha mapenzi kwa Simba SC.

Aliyekuwa winga wa klabu ya Simba SC, Benard Morrison
Image: Instagram

Aliyekuwa mchezaji wa timu ya soka ya Simba nchini Tanzania, winga Bernard Morrison ameashiria kwamba timu hiyo alikuwa anaipenda sana ila imemkatisha tamaa sana kwa kuusitisha mkataba waka ghafla.

Ikumbukwe mnamo mwezi Mei, timu ya Simba ilitoa taarifa kwa umma kwamba imempa likizo ya lazima mchezaji huyo nguli kutokea Ghana hadi mwishoni wa msimu, msimu ambao umekamilika wikendi iliyopita.

Katika taarifa ambayo ilitolewa kwa umma wiki sita zilizopita, klabu hiyo ilisema kwamba maafikiano yaliafikiwa kutoka pande zote mbili kwamba Morrison alikuwa apewe nafasi ya kupumzika ili kushughulikia mambo yake ya kibinafsi.

Aidha kwa kile kilichoonekana kama ni mwisho wa mchezaji huyo kuiwajibikia klabu ya Simba, taarifa hiyo ilizidi kusema kwamba inamshukuru Morrison kwa mchango wake kipindi chote alikuwa anaitumikia timu uwanjani na kumtakia kila la kheri katika mapumuziko yake na safari yake ya soka baadae.

Wengi walisema tu kwamba ni njia moja ya timu hiyo kushiba huduma ya Morrison na katika mahojiano ya kipekee na mchambuzi wa soka, Morrison alisema kwamba mkurugenzi mkuu wa timu alimwambia kwamba wachezaji wenzake tu ndio hawamtaki na hivyo kumtaka akae mbali na timu ya Simba.

“CEO aliniita ofisini kwake akaniambia wachezaji wengine hawanitaki kwa hiyo nikae mbali na timu. Nikamwambia mbona wananipenda na tulikuwa tunacheka nao muda mrefu! kama kuna mwingine sema lakini labda hilo la kuchukiwa na wenzangu sio kweli. Akaniambia nenda utulie nitakujulisha,” Alisema Morrison katika mahojiano ya runinga moja nchini humo.

Pia alizidi kutema nyongo kwamba kwa kuwa alikuwa kipenzi cha mashabiki wengi wa timu ya Simba, alishrutishwa kukubali moja kati ya mawili ambapo ilikuwa akubali kwamba ana matatizo ya kifamilia ili mashabiki wajulishwe kuhusu lengo la hiyo likizo ama mkataba wake kukatishwa kabisa. Ilimbidi kuchagua likizo ya matatizo ya kifamilia kwa kuwa kusimamishwa kungemchafulia jina.

Juzi msimu wa ligi kuu ya NBC ilipokamilika na watani wao wa jadi, Yanga kutawazwa mabingwa, Morrison alitema ya moyoni ambapo aliandika kwamba Simba imemtamausha sana japokuwa alikuwa anaipenda na kuitumikia timu kwa moyo na ari ila ndio hivyo tena hawahitaji huduma zake tena uwanjani.

Morrison alidokeza kwamba hivi karibuni anarudi zake Ghana na kuwataka mashabiki wa Simba kumpa zawadi ya jezi mia moja ili kuwagawia mashabiki wake nchini kwao kama njia moja ya kuonesha upendo wake kwa timu ya Simba.

“Mara nyingi tunakatishwa tamaa na wale tunaowapenda na kuwaamini. Lakini wacha nifanye hadithi kuwa fupi na rahisi, nahitaji vipande 100 vya jezi za Simba kutoka kwa mashabiki waaminifu ili zipewe marafiki na familia nchini Ghana. Hii ni kutokana na mashabiki wengi kuniaga kwa sababu nitakatishwa tamaa ikiwa nitaendelea kusubiri moja kutoka kwa klabu yangu. Tafadhali andika jina lako nyuma na namba 3. Anyone interested can bring to me at sea breeze Mbezi beach,” aliandika Morrison kwenye Instagram yake.