Cristiano Ronaldo aomba kuondoka Manchester United

Muhtasari

•Ronaldo anataka Manchester United kumwachilia aondoke katika klabu hiyo iwapo watapata ofa bora.

•Ronaldo aligombana na Harry Maguire katika nafasi ya unahodha wa United msimu uliopita.

Manchester United imebanduliwa kutoka Champions League
Manchester United imebanduliwa kutoka Champions League
Image: GETTY IMAGES

Cristiano Ronaldo anataka Manchester United kumwachilia aondoke katika klabu hiyo iwapo watapata ofa bora kwa ajili yake msimu huu wa joto.

Mshambuliaji huyo wa Ureno, 37, alirejea Old Trafford kutoka Juventus msimu uliopita wa joto.

Hata hivyo, licha ya kuwa mfungaji bora wa United msimu uliopita - na wa tatu katika Premier League - kampeni yote kwa jumla ilionekana kuwa ya kukata tamaa .

United walimaliza katika nafasi ya sita kwenye ligi ya Premier  hivyo wakakosa kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa.

Hiyo ina maana kwamba Ronaldo, ambaye amesalia na mwaka mmoja kwenye mkataba wake na United pamoja na mwaka wa hiari, atacheza katika Ligi ya Europa kwa mara ya kwanza.

Sio kitu anachofurahia na mshindi huyo mara tano wa tuzo ya Ballon d'Or anahisi kunaweza kuwa na chaguo la kuvutia zaidi katika kipindi hiki katika maisha yake ya soka.

Mchezaji huyo atasalia Mancheter United licha ya kuhusishwa na uhamisho wa kujiunga na Chelsea.

Fowadi huyo wa zamani wa Real Madrid ana wasiwasi akisisitiza kuwa anaiheshimu United lakini anapoingia katika hatua za mwisho za maisha yake ya soka, anataka kuwania tuzo kubwa zaidi.

United bado haijasema lolote kuhusu mustakabali wa Ronaldo, ingawa awali vyanzo vya habari viliamini kwamba Mreno huyo angesalia Old Trafford msimu ujao.

Ingawa itakuwa pigo kwa United ikiwa wangempoteza mmoja wa wachezaji bora zaidi ambao wamewahi kuwa nao, pia ingesuluhisha maswala machache kwa meneja mpya Erik ten Hag.

Ronaldo aligombana na Harry Maguire katika nafasi ya unahodha wa United msimu uliopita, huku hamu ya kocha wa muda Ralf Rangnick ya kutekeleza mtinfo wake ikizimwa na Ronaldo aliyekataa kushiriki katika mfumo kama huo.

Ingawa Ten Hag amesema ni kwa kiasi gani anatazamia kuungana na Ronaldo, haijabainika ni kwa namna gani uchezaji wa fowadi huyo utaendana na Mholanzi huyo.

Zaidi ya hayo, Ronaldo ndiye mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi kwenye Ligi Kuu ya England na kuondoka kwake kungeleta wigo zaidi ndani ya bajeti ya United ya msimu wa joto.

Ronaldo anatarajiwa kurejea klabuni hapo kwa mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya wiki hii. Inatarajiwa atakuwa kwenye ziara yao ya maandalizi ya msimu mpya nchini Thailand na Australia.