AFCON: Fainali za 2023 zasogezwa hadi 2024- kunani?

Muhtasari

•Michuano hiyo ilitarajiwa kuandaliwa kati ya mwezi Juni na Julai 2023 ambacho ndio kipindi cha mvua nchini Ivory Coast.

Image: BBC

Kombe la mataifa ya bara Afrika litachezwa nchini Ivory Coast 2024 na sio 2023, Rais wa shirikisho la soka barani Afrika {Caf} Patrice Motsepe alisema siku ya Jumapili.

Michuano hiyo ilitarajiwa kuandaliwa kati ya mwezi Juni na Julai 2023 ambacho ndio kipindi cha mvua nchini Ivory Coast.

‘’Hatuwezi kuhatarisha’’ , alisema raia huyo wa Afrika Kusini katika mji mkuu wa Rabat.

Huku Kombe la Dunia nchini Qatar likitarajiwa kufanyika mwezi Novemba  na Disemba , uamuzi huo umechukuliwa kuahirisha fainali hizo badala ya kuziandaa katika tarehe ya mbele.

Hiyo ina maana kwamba kombe hilo la mataifa ya Afrika litaandaliwa mwezi Januari au February kwa mara ya pili mfululizo baada ya kombe hilo kuchezwa mwaka huu nchini Cameroon.

Mwaka 2017, Caf ilitangaza kwamba itabadili fainali hizo kuchezwa mwezi Juni na Julai badala ya mwezi Januari na februari kama inavyokuwa , ili kuzuia mizozo ya mara kwa mara huku klabu za Ulaya zikilazimika kuwaachilia wachezaji katikati ya msimu.

‘’Januari sio wakati mwafaka kwasababu ya vilabu vya Ulaya , lakini ndio chaguo la pekee tulilonalo’’, aliongezea Motsepe.