Gor yamfuta kazi kocha Spiers miezi sita baada ya kumpa kandarasi

Timu mbalimbali zimewafuta kazi makocha wao ikiwemo Simba ya Tanzania, PSG ya Ufaransa na sasa Gor ya Kenya.

Muhtasari

• Spier alijiunga na vigogo hao wa soka la humu nchini mnamo mwezi Februari ambapo Gor ilimpa kandarasi kama mkufunzi mkuu

Aliyekuwa meneja mkuu wa Gor Mahia, Andreas Spier
Gor Mahia Aliyekuwa meneja mkuu wa Gor Mahia, Andreas Spier
Image: Facebook

Timu ya mpira wa miguu nchini Kenya, Gor Mahia kwa mara nyingine tena imemfuta kazi kocha mkuu Mjerumani Andreas Spier baada ya kuhudumu kama mkufunzi klabuni humo kwa miezi sita tu!

Kupitia taarifa rasmi iliyoandikwa kwenye ukurasa wa facebook wa timu hiyo Jumanne alasiri, Gor walidhibitisha kwamba Spier si kocha wao tena ka kusema kwamba ameondoka baada ya kandarasi yake ya miezi sita kukamilika.

“Tunaweza kuthibitisha kwamba tumemaliza mkataba na kocha mkuu Andreas Spiers. Mkataba wake uliisha na sasa tuko sokoni kutafuta kocha mpya. Tunamtakia kila la heri,” sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.

Timu ya Gor Mahia ambayo imekuwa ikivurunda kwa misimu ya hivi karibuni inasemekana kuwaajiri na kisha kuwafuta kazi makocha zaidi ya wanane tangu mwaka huu ulioanza.

Spier alijiunga na vigogo hao wa soka la humu nchini mnamo mwezi Februari ambapo Gor ilimpa kandarasi kama mkufunzi mkuu huku akisaidiwa na Michael Nam katika safu ya kiufundi ya timu hiyo.

Kocha Spier anajulikana katika ukanda wa Afrika mashariki kwa kuiongoza timu ya APR ya Rwanda hadi kutwaa ubingwa wa ligi kuu nchini humo kati ya mwaka wa 2013-2014.

Awali, kocha Andreas Spier alifanya kazi nchini Kenya katika shirikisho la soka FKF, alipohudumu kama mkurugenzi wa kiufundi, kitengo ambacho alifanikisha shughuli nyingi na timu ya taifa ya vijana wasiozidi umri wa miaka 18.

Mjerumani huyo ambaye ana leseni ya kuhudumu kama kocha mkuu kutoka kwa shirikisho la soka barani uropa, UEFA, pia amewahi kuwa mkurugenzi wa kiufundi wa shirikisho la soka nchini Rwanda, FERWAFA.

Ama kweli ni ule msimu wa timu kufanya mabadiliko katika safu zao za ukufunzi, si tu barani Afrika bali hata Uropa ambapo vibarua vya wakufunzi vinazidi kuingiwa doa na kuota nyasi kweli kweli.