Romelu Lukaku: Nilifanya makosa makubwa kurudi Chelsea!

Lukaku kwa sasa yupo Inter Milan kwa mkopo akitokea Chelsea.

Muhtasari

• Mchezaji huyo alifichua kwamba hata baada ya kuigura Inter, hakushawishika kuuza nyumba yake kwani alijua angerudi kule tu.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Belgium Romelu Lukaku amabye anaisakatia Inter Milan kutoka Chelsea
Mshambuliaji wa kimataifa wa Belgium Romelu Lukaku amabye anaisakatia Inter Milan kutoka Chelsea
Image: The Star (Maktaba)

Mchezaji wa Chelsea na ambaye amerejea katika timu ya Inter Milan kwa mkopo, Romelu Lukaku kwa mara nyingine amezua mjadala mkali kwenye tasia ya soka baada ya kudai kwamba yalikuwa ni makosa makubwa kujiunga na timu ya Chelsea.

Alisema kwamba hata baada ya kushawishiwa kujiunga na timu hiyo yake ya utotoni kutoka Inter Milan, bado hakuridhia kuuza nyumba yake nchini Uitaliano kwa sababu alikuwa na hisia kwamba siku moja angerudi huko.

Baada ya kurudi Milan, Lukaku alisema kwamba amerudisha furaha yake tena baada ya msimu mmoja wa kiza akiisakatia Chelsea ya Uingereza.

“Sasa nina furaha kuvaa jezi hii, timu inajua tunachohitaji kufanya, itakuwa changamoto kubwa msimu huu na tunahitaji kuendelea hivi. Niligundua msimu uliopita nilipokuwa Uingereza, jinsi Inter walivyo muhimu duniani,” mchezaji huyo alisema kulingana na taarifa zilizochapishwa na jarida la The Sun.

Lukaku alianza fani yake ya usakataji kwenye klabu ya Chelsea baada ya kuenda kwa mkopo katika timu mbali mbali ambapo Everton walimnunua na kisha baadae kuihamia Manchester United.

Akiwa Manchester United mambo hayakumkubali vile ambapo aligura na kuelekea Uitaliano kujiunga na Inter Milan ambapo alijizolea heshima kocho kocho kwenye midomo ya wapenzi wa mchezo huo wenye ufuasi mkubwa duniani.

Chelsea baada ya kuwa na ukame wa magoli waliamua kutafuta mshambuliaji ambapo waliafikia uamuzi wa kumrudisha Lukaku ugani Stamford Bridge mwanzoni mwa msimu jana katika rekodi ya milioni $117 lakini matarajio yake katika klabu ya Chelsea yalikwenda mrama pale ambapo alijipata kuzomewa vikali na mashabiki kwa kushindwa kutatua tatizo la ufungaji mabao linalowakumba miamba hao wa London.

Kwa sasa Lukaku amehamia Inter Milan ambapo amesema ni kama furaha yake imerejea na haona uwezekano wa kurudi tena Chelsea, huenda akalazimisha mkopo wake kuwa uhamisho wa rasmi huko Milan.