Bernd Leno awaaga Wanabunduki baada ya miaka minne

Leno alisajiliwa na Fulham kwa pauni milioni 8 na kutia saini mkataba wa miaka mitatu.

Muhtasari

•Leno ambaye ana umri wa miaka 30 anaripotiwa kuigharimu Fulham pauni milioni 8 na alitia saini mkataba wa miaka mitatu.

•Leno alitoa shukran za dhati kwa klabu, wachezaji wenzake, wafanyikazi na mashabiki kwa ushirikiano mwema.

Image: TWITTER// BERND LENO

Mlinda lango wa Ujerumani Bernd Leno amekamilisha uhamisho kutoka klabu ya Arsenal na kujiunga na Fulham.

Fulham ilimzindua Leno kama mchezaji wake mpya Jumanne usiku baada ya kukamilika kwa vipimo vya kidaktari.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 anaripotiwa kuigharimu klabu hiyo ya West London pauni milioni 8 na alitia saini mkataba wa miaka mitatu.

Leno alijiunga na Arsenal kutoka  Bayer Leverkusen takriban miaka minne iliyopita na kuichezea klabu hiyo kwa misimu minne. Katika kipindi  hicho alishirikishwa kwenye mechi 125 na kutofungwa katika mechi 16.

"Tunakushukuru Bernd kwa mchango wako kwa klabu katika miaka minne ambayo umekuwa nasi. Kila mtu katika Arenal anamtakia Bernd na familia yake mafanikio katika ukurasa wao mpya," Taarifa ya Arsenal ilisoma.

Mlinda lango huyo ambaye amejizolea upendo mkubwa kutoka kwa mashabiki katika misimu minne iliyopita alisema amefurahia kipindi chake pale.

Alitoa shukran zake kwa klabu, wachezaji wenzake, wafanyikazi na mashabiki kwa ushirikiano mwema ambao umekuwepo.

"Habari mashabiki wa Arsenal, ni wakati wa kuendelea kwa ajili yangu. Imekuwa ni furaha kuwa sehemu ya klabu hii kubwa ya soka kwa miaka 4 ya ajabu. Asante sana kwa support yenu. Pia asante kubwa kwa wachezaji wenzangu na wafanyikazi nyuma ya timu. Natarajia kuwaona hivi karibuni!" Leno alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Mjerumani huyo alianza kukosa dakika tosha langoni  baada ya Arsenal kupata huduma za Aaron Ramsdale msimu uliopita.

Ramsdale ambaye ana umri wa miaka 24 alihusishwa katika mechi zaidi za klabu hiyo katika msimu wa 2021/22.