Sadio Mane atuma vifurushi 150 vya chokoleti kwa wafanyikazi wa Liverpool kama shukrani

Katika kila kifurushi kulikuwepo na picha yake na ujumbe wa kauli mbiu ya timu hiyo "You'll Never Walk Alone"

Muhtasari

• Mane aliwatumia wafanyikazi wote wa Liverpool chokoleti kama shukrani kwa kukaa nao kwa miaka 6 kabla ya kugura kwenda Bayern Munichen.

Mshambulizi wa Bayern Munich na Senegali, Sadio Mane
Mshambulizi wa Bayern Munich na Senegali, Sadio Mane
Image: Facebook//Sadio Mane

Katika historia soka kote ulimwenguni, unapozungumzia wachezaji wenye nidhamu kubwa na ukarimu wa hali ya juu basi jina la mshambulizi wa Bayern Munichen Sadio Mane litatajwa kwa herufi za dhahabu.

Mchezaji huyo ambaye aliondoka Liverpool mapema msimu huu hajawasahau mashabiki wa timu hiyo iliyomkuza kwa takribani miaka sita kwani inaarifiwa amewatumia wafanyikazi wa timu hiyo wapatao 150 viroba vya biskuti za chokoleti kama shukrani zake kwa wafanyakazi kutoka sekta zote za klabu, kulingana na ripoti kutoka kwa Christian Falk.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 aliondoka Anfield na kuelekea Bayern msimu huu wa joto kwa pauni milioni 35, na tayari ameanza kupata mafanikio yake katika klabu hiyo mpya baada ya kufunga mabao mawili katika mechi tatu akiwa na kikosi hicho cha Bundesliga.

Christian Falk alifichua kitendo cha ukarimu cha mchezaji huyo kwenye Twitter, akiandika: “Sadio Mane anatuma vifurushi 150 vya chokoleti kwa wafanyakazi wa Liverpool, Kutoka kwa mtu wa kusafishaji hadi mlinzi, kila mtu anapata chokoleti yenye picha ya Sadio na kadi iliyoandikwa na mchezaji huyo”

Ndani ya kila kadi iliandikwa kauli mbiu ya klabu: 'Hautatembea Peke yako.'

Katika misimu sita iliyobeba mataji na Wekundu hao, fowadi huyo wa Senegal alishinda karibu kila taji, ikiwa ni pamoja na Ligi Kuu, Ligi ya Mabingwa, UEFA Super Cup, na Kombe la FA na Carabao.