Kila mara nawaza kuhusu mlo unaofuata kwa watu kijijini mwetu Senegal - Sadio Mane

Fikira hizo ndizo zinampa motisha wa kufanya bidii uwanjani ili asipoteze nafasi yake na kushindwa kuwahudumia watu.

Muhtasari

• “Sijioni bora kuliko mtu yeyote. Ninakwenda tu uwanjani na kufanya kazi yangu vizuri" - Sadio Mane.

• Mane ni mmoja wa wachezaji wenye roho nzuri katika kizazi hiki ambao wanazungumziwa sana kwa ukarimu wao wa kujitoa kwa watu ili kutia tabasamu nyusoni mwao.

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Senegal, Sadio Mane
Image: Frank Khalid (Twitter)

Mfanyibiashara na mfuatiliaji wa masuala ya soka la Uropa, Frank Khalid kupitia ukurasa wake wa Twitter amepakia nukuu moja kutoka kwa mchezaji wa timu ya taifa ya Senegali na mshambuliaji wa Bayern Munich Sadio Mane kuhusu ni kwa nini anataka kuendelea kucheza.

Kulingana na nukuu hiyo yenye kugusa sana kwa huruma, Mane anasema kwamba yeye katika maisha yake na pia wakati anapoingia uwanjani siku zote ndani ya kichwa chake huwa anawafikiria watu wa taifa lake wanaoishi katika hali ngumu ya umaskini na ndio maana anapambana kila uchao ili kuhakikisha anadumisha ubora wake ili aendelee kulipwa na kuwasaidia watu wa nyumbani kwao Senegali.

Mane ananukuliwa akisema kwamba yeye haingii uwanjani kwa dhana ya kujiona bora zaidi ya mchezaji mwingine bali muda wote kichwa chake kimekumbwa na fikira za watu wake na chakula watakachokila baadae amabcho aghalabu hakipo na wao hukipata kwa tabu na jasho kubwa.

Kulingana na kauli hiyo, fikira za namna hii ndizo zinampa msukumo wa kutia bidi katika mazoezi na pia uwanjani ili asipoteze nafasi yake katika kikosi.

“Sijioni bora kuliko mtu yeyote. Ninakwenda tu uwanjani na kufanya kazi yangu vizuri. Mimi huwa na wasiwasi kila mara kuhusu mlo unaofuata kwa ajili ya watu wa kijiji changu huko Senegali. Hii ndio sababu lazima niwe katika kiwango bora kila wakati ili nisipoteze nafasi yangu,” Sadio Mane ananukuliwa na Frank Khalid.

Mane ni mmoja wa wachezaji wenye roho nzuri katika kizazi hiki ambao wanazungumziwa sana kwa ukarimu wao wa kujitoa kwa watu ili kutia tabasamu nyusoni mwao.

Kwa wakati mmoja, iliwahi kusemekana kwamba mchezaji huyo anamiliki simu bovu yenye kioo kilichochanika licha ya kuwa na posho nene kutoka mitikasi yake ya kisoka lakini yeye alisema kwamab haoni Fahari katika kumiliki vitu vya thamani ilhali watu wa kwao wanaishi maisha mabaya na ndio maana pesa zake nyingi aliziwekeza kujenga hospitali na kiwanja cha michezo nyumbani kwao Senegali.