Pogba asema analengwa na genge la uhalifu wa kupangwa

Polisi wa Ufaransa wameanzisha uchunguzi.

Muhtasari

•Kiungo huyo wa Juventus na Ufaransa alitoa taarifa kupitia kwa mawakili wake siku ya Jumapili akisema suala hilo limeripotiwa kwa mamlaka.

•Hapo awali, kakake Pogba Mathias alichapisha video mtandaoni akiahidi kuchapisha "ufichuzi mkubwa" kuhusu mchezaji huyo.

Image: BBC

Paul Pogba anasema amekuwa akilengwa na unyang'anyi na vitisho kutoka kwa genge la uhalifu wa kupangwa .

Kiungo huyo wa Juventus na Ufaransa alitoa taarifa kupitia kwa mawakili wake siku ya Jumapili akisema suala hilo limeripotiwa kwa mamlaka.

Shirika la habari la AFP, likinukuu chanzo, lilisema polisi wa Ufaransa wameanzisha uchunguzi.

Hapo awali, kakake Pogba Mathias alichapisha video mtandaoni akiahidi kuchapisha "ufichuzi mkubwa" kuhusu mchezaji huyo.

Mathias Pogba alisema taarifa hizo huenda zikawa "mlipuko", bila kutoa maelezo zaidi.

"Ni pamoja na vitisho na majaribio ya unyang'anyi ya genge lililopangwa dhidi ya Paul Pogba," ilisema taarifa hiyo.

"Mashirika yenye uwezo nchini Italia na Ufaransa yalifahamishwa mwezi mmoja uliopita na hakutakuwa na maoni zaidi kuhusiana na uchunguzi unaoendelea."

Mshindi huyo wa Kombe la Dunia akiwa na Ufaransa mwaka 2018, Pogba alihamia Juventus kwa uhamisho wa bure msimu huu baada ya kuondoka Manchester United.

Katika video zake, Matthias Pogba alisema "ulimwengu mzima, pamoja na mashabiki wa kaka yangu, na hata zaidi timu ya Ufaransa na Juventus, wachezaji wenza wa kaka yangu na wafadhili wake wanastahili kujua mambo fulani".

Alisema ufichuzi huo utahusisha wakala wa Pogba, Rafaela Pimenta.