Ni nini Hatma ya ligi kuu EPL baada ya kifo cha malkia Elizabeth II?

Malkia Elizabeth wa pili alifariki usiku wa jana akiwa na umri wa miaka 96.

Muhtasari

• Uingereza ilitangaza siku kumi na mbili za maombolezo kufuatia kifo cha malkia huyo aliyehudumu katika ikulu ya Buckingham kwa miaka 70.

Wachezaji katika ligi ya EPL wamkumbuka malkia Elizabeth 2
Wachezaji katika ligi ya EPL wamkumbuka malkia Elizabeth 2
Image: BBC SPORT

Baada ya kifo cha Malkia Elizabeth wa pili katika ufalme wa Uingereza, sasa kuna sintofahamu miongoni mwa wadau wa soka huku baadhi wakibaki katika njia panda kuhusu uwezekano wa kuendelea au kusitishwa kwa shughuli zote za spoti nchini humo.

Wapenzi wa soka la Uingereza EPL kote duniani huenda wakalazimika kujivinjari kwa michezo mingine. Hii ni baada ya madai kuzuka kwamba michezo Uingereza huenda itasitishwa kutokana na kifo cha malkia huyo ili kumpa heshima zake za mwisho.

Baada ya ikulu ya Buckingham kutangaza usiku wa Alhamis kwamba taifa hilo babe duniani litachukua siku 12 za maombolezi ambapo shughuli zote za kuwakusanya watu pamoja zikisitishwa.

Baadhi ya shughuli zilizopigwa breki ni pamoja na michezo yote ya kila aina, mikutano ya kisiasa na mikusanyiko ya hafla za kuchekesha miongoni mwa shughuli nyingine tumbi nzima.

Kulingana na jarida la Football London, kuna uwezekano mkubwa kwamba mechi za wikiendi hii za Ligi Kuu ya Uingereza ambazo zilikusudiwa kuanza na London Derby kati ya Fulham na Chelsea, zitasitishwa.

Ligi kuu ya Uingereza inatarajiwa kutoa taarifa rasmi hivi karibuni. Bodi ya Kriketi ya Uingereza na Wales tayari imeahirisha siku ya pili ya Mchuano wa Tatu kati ya Uingereza na Afrika Kusini. Ziara ya DP pia imethibitisha kuwa Mashindano ya Gofu ya BMW PGA pia yamesimamishwa.

Jarida hilo lilikisia kwamba huenda shughuli zote zikasitishwa kama ambavyo ilifanyika mwaka 1997 wakati Princess Diana alipofariki kwa ajali.

“Kufuatia kifo cha Princess Diana mnamo Jumapili Agosti 31 mwaka 1997, mechi ya Ligi Kuu ya Liverpool dhidi ya Newcastle United iliyopangwa kuanza baadaye siku hiyo iliahirishwa. Ratiba ya Ligi ya Soka wikendi iliyofuata ilisukumwa ili kuepusha mgongano na mazishi ya Diana. Ligi kuu ya Uingereza ilikuwa kwenye mapumziko ya kimataifa,” jarida la Football London liliibua kumbukumbu.