MATOKEO MAZURI

K'Ogalo yapewa kichapo na Posta baada ya kuadhibu Talanta

K'Ogalo walicharaza Talanta mabao 3-1 katika mechi ya kirafiki kwenye uga wa Camp Toyoyo mjini Nairobi siku ya Jumamosi.

Muhtasari

•Mshambulizi Peter Lwasa alitikisa nyavu kwa mkwaju wa penalti kabla ya Benson Omala kufunga bao la pili na kuhitimisha ushindi huo.

•Gor Mahia wana hamu ya kutwaa taji lao la 20 la ligi kuu baada ya kusalia kwenye baridi kwa misimu miwili.

Mechi ya kirafiki kati ya Gor Mahia na Posta Rangers iliyoandaliwa kwenye uwanja wa Camp Toyoyo.
Mechi ya kirafiki kati ya Gor Mahia na Posta Rangers iliyoandaliwa kwenye uwanja wa Camp Toyoyo.
Image: GOR MAHIA FACEBOOK

Kocha mkuu wa Gor Mahia Johnathan McKinstry, amesema wataendelea kunoa makucha katika mechi za kirafiki huku wakijiandaa kutwaa tena taji la Ligi Kuu ya Kenya msimu ujao.

Mkufunzi huyo alizungumza baada ya timu yake kurekodi matokeo mchanganyiko katika mechi zao mbili za kirafiki zilizochezwa wikendi.

Katika mechi yao ya kwanza Jumamosi, K'Ogalo iliilaza Talanta 3-1 katika uwanja wa Camp Toyoyo jijini Nairobi lakini ikashindwa katika uwanja huo huo na Posta Rangers ambao walifunga bao lao la pekee kupitia kwa mchezaji Eliud Lokuwam.

Dhidi ya Talanta, mshambulizi Peter Lwasa alifunga kupitia mkwaju wa penalti kabla ya mabao mawili ya Benson Omala kuhitimisha ushindi huo muhimu.

“Nilifikiri ilikuwa mechi nzuri kwa timu zote kwa sababu kucheza dhidi ya wapinzani wenzako wa Ligi Kuu ya Kenya kunamaanisha kuwa kuna ushindani katika mechi hizo," McKinstry alisema.

"Lengo kuu la mchezo ni kujiandaa kwa msimu ujao. Nilidhani tuliona mambo mazuri kutoka kwa Gor lakini pia bado kuna mambo ya kufanyia kazi kwa hivyo ni hatua nyingine katika safari yetu,” akasema kocha huyo.

McKinstry, ambaye alichukua nafasi ya mtaalamu wa Ujerumani Andreas Spier miezi miwili iliyopita, alionyesha kuridhishwa na matokeo ya mechi hiyo.

Gor Mahia wana hamu ya kutwaa taji lao la 20 la ligi kuu baada ya kusalia kwenye baridi kwa misimu miwili.