(+video) "Salasya na mpira!" Mbunge wa Mumias East ajiunga na timu ya Bunge FC

Mbunge huyo aliahidi kuiwakilisha timu yake kwa hali na mali.

Muhtasari

• Alisema kwamba atawakanyaga vibaya sana wapinzani wao pindi watakapokutana uwanjani na atafunga mabao mengi zaidi.

Mbunge wa Mumias East Peter Salasya amekuwa sajili mpya katika kikosi cha soka cha Bunge. Mbunge huyo ambaye ni mzungumzaji sana katika mahojiano ya blogu na vyombo vya habari alipasua mbarika habari hizo kupitia mitandao yake ya kijamii.

Katika video ambayo aliipakia TikTok na kisha kuipakia tena Tweeter, Salasya alizua mzaha kwamba timu ya soka ya Bunge FC imekuwa yenye bahati kupata mkataba wake ambapo alijiita kama mshambuliaji matata sana atakayenongeza nguvu katika kiungo cha ushambuliaji kwenye timu hiyo ya Wabunge.

Alisema kwamba atawakanyaga vibaya sana wapinzani wao pindi watakapokutana uwanjani na atafunga mabao mengi zaidi kuliko wachezaji nguli katika soka la Ulaya.

“Bunge la Kitaifa nchini Kenya, timu ya Bunge FC leo nimesajiliwa kuwa mshambuliaji mpya munoma sana kutoka wanga. Mheshimiwa Salasya amejitolea kuipa nguvu timu kwa ukuu na ubora wake. Nimeshaingia kwenye timu rasmi, nataka kukanyaga hawa watu,” Salasya alisema.

Mbunge huyo katika wasilisho lake la kwanza bungeni wiki mbili zilizopita, alizua vichekesho baada ya kumtambua naibu spika ambaye ni wa kike kwa jina la kiume kwa kujiradidi hata baada ya kurekebishwa.

Waziri mteule wa usalama Aden Duale alimsuta vikali akisema kwamba hawezi kuwa mbunge katika bunge la kitaifa lenye watu wa heshima, jambo ambalo Salasya alimshtumu vikali kwa kujibu mipigo.