(+video) Mourinho akwepa kadi nyekundu kimtindo, atoroka kimya kimya kutoka kwa refa

Kocha huyo alikuwa anaharakisha kufika kwa refa akizua lakini alipoona kadi nyekundu mkononi mwa refa, alikata kona na kurudi alikotoka.

Muhtasari

• Zogo lilizuka baina ya wachezaji wake na wa Napoli baada ya mechi kukamilika.

• Mourinho alionekana kutaka kuingilia kati zogo hilo ila alipoona kadi nyekundu mkononi mwa refa, aligeuka kimpango na kutoroka.

Video moja inayosambaa mtandaoni inaonyesha kocha wa AS Roma Jose Mourinho akikwepa kwa mshangao hali ya kuonyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa mechi ya timu yake dhidi ya Napoli.

Mechi hiyo iliyokuwa na upinzani mkali iliisha kwa faida ya Napoli, baada ya mshambuliaji matata kutoka Nigeria Victor Osimhen kufunga bao moja na la ushindi kunako dakika ya 80 kabla ya mchezo kumalizika.

Katika video hiyo ambayo imezua vichekesho mitandaoni, zogo lilizuka baada ya kipenga cha mwisho wakati mchezaji mmoja wa Roma alipomtuhumu refa kwa kumkanyaga mguuni.

Baada ya mchezaji huyo kumkaripia vikali refa, alitoa kadi nyekundu mfukoni na kuishika mkononi kwa nyuma huku akisubiria mchezaji atakayeendelea kumkaripia zaidi na kumuonesha kadi hiyo ya kumfungia nje ya michezo mitatu ijayo.

Wakati hayo yakiendelea na refa akiwa ameshikilia kadi nyekundu tayari kumuinulia yeyote atakayemfika kooni, kocha Mourinho alionekana akijaribu kuingilia kati suala hilo huku akija mbio upande wa refa.

Alipofika karibu na refa aliona mkononi kuna kadi nyekundu na kocha huyo alionekana akipinda na kukata kona kabla ya kurudi alikotoka, hivyo kukwepa kurambishwa kadi nyekundu.

Wengi walioona video hiyo walisema kwamba kocha huyo mbwatukaji huenda amejifunza kutokana na matukio ya awali ambapo alijaribu kuingilia kadi kukaripiana na refa, tukio lililomsababishia kuoneshwa kadi nyekundu na kuzuiliwa kuhudhuria mechi za timu yake.