Sadio Mane apeana zawadi ya jezi 100 za Bayern kwa watoto maskini Senegal

mchezaji huyo alionekana akisaini jezi hizo na kuzipeana zisafirishwe hadi Senegal ambapo watoto maskini walionekana wakizipokea.

Muhtasari

• Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 amefunga mabao 10 katika mechi 20 katika mashindano yote kwa The Bavarians.

Sadio Mane atoa jezi 100 kwa watoto maskini
Sadio Mane atoa jezi 100 kwa watoto maskini
Image: Instagram, Twitter

Wahenga wenye midomo walisema, njia pekee ya kuishi kwa furaha na Amani ya nafsi, ni kuzidisha kupeana kama njia ya msaada na wala si kuzidi kupokea!

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Senegali na klabu ya Ujerumani ya Bayern Munich ameendeleza msururu wa ukarimu wake baada ya kutoa jezi zaidi ya mia za klabu hiyo ili kupeanwa kama zawadi kwa watoto maskini nyumbani kwao Senegali.

Mchezaji huyo katika video iliyopakiwa kwenye mitandao ya kijamii alionekana akizisaini jezi hizo za Bayern Munich na kuzipeana kwa wanahabari waliokuwa wakisafiri kuenda Senegali kuzipeana kwa watoto maskini wenye ndoto za kuwa wachezaji katika kitongoji cha Bambali, Senegali.

Fowadi huyo wa Senegal amekuwa mpokeaji wa kwanza wa Tuzo ya Socrates katika tuzo za Ballon d'Or mwezi uliopita kutokana na kazi zake nje ya uwanja.

Kama sehemu ya filamu iliyoandaliwa na waandishi wa habari wa TNT huko Bambali, timu ya wanahabari hao ilisafiri kwa ndege hadi Senegal kutoa jezi hizo kwa watoto maskini.

Wanahabari hao walifika na kuonekana wakigawa jezi hizo kwa watoto waliopokea kwa furaha na kuzivaa papo hapo huku rangi za zambarau ambayo ni ya Bayern Munich ikihanikiza Bambali.

Mane alijiunga na Bayern Munich katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi akitokea Liverpool na tangu wakati huo amekuwa na kampeni ya kipekee katika kuwatumikia miamba hao wa Ujerumani.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 amefunga mabao 10 katika mechi 20 katika mashindano yote kwa The Bavarians.