Southampton yamtimua meneja wake mkuu Ralph Hasenhuttl

Klabu hiyo imesema inahisi kuwa sasa ni wakati mwafaka wa mabadiliko.

Muhtasari

•Ralph ,55, anaondoka katika klabu hiyo baada ya kuhudumu kama meneja mkuu kwa takriban miaka minne.

•Kutimuliwa kwa Ralph kunajiri masaa machache tu baada ya Southampton kuchapwaha 1-4 na Newcastle.

Ralph Hasenhuttl
Image: TWITTER// SOUTHAMPTON

Klabu ya Southampton imemfuta kazi meneja wake mkuu Ralph Hasenhuttl  pamoja na msaidizi wake Richard Kitzbichler.

Southampton ilithibitisha kutimuliwa kwa Ralph siku ya Jumatatu na kusema inahisi kuwa sasa ni wakati mwafaka wa mabadiliko.

"Kila mtu anayehusika na klabu angependa kutoa shukrani zao za dhati kwa Ralph kwa jitihada zake zote, pamoja na kujitolea kwake bila kuyumbayumba katika muda wake wote kama meneja," taarifa ya klabu hiyo ilisoma.

Ralph ,55, anaondoka katika klabu hiyo baada ya kuhudumu kama meneja mkuu kwa takriban miaka minne.

Kocha mkuu wa kikosi cha kwanza cha klabu hiyo, Ruben Selles, atachukua usukani kutoka kwa Ralph kwa muda huku klabu ikiendelea kutafuta mridhi wa raia huyo wa Austria.

Kutimuliwa kwa Ralph kunajiri masaa machache tu baada ya Southampton kupokea kichapo cha 1-4 kutoka kwa Newcastle.

Klabu hiyo imekuwa ikiandikisha msururu wa matokeo hafifu msimu huu huku ikiwa imejizolea pointi 12 katika mechi 12 ambazo imecheza kufikia sasa.

Kwa sasa The Saints wanashikilia nafasi ya 18 kati ya klabu 20 zinazoshiriki ligi kuu ya EPL.