Southampton yamteua kocha mpya baada ya kumtimua Hasenhuttl

"Ninajivunia sana kupewa nafasi hii," alisema Jones.

Muhtasari

•Jones, 49, ameondoka kwenye klabu ya Championship ya Luton Town na kuchukua jukumu hilo kwa kandarasi ya miaka mitatu unusu.

•Jukumu la kwanza la Jones litakuwa wikendi hii ambapo The Saints watasafir hadi ugani Anfield kumenyana na Liverpool.

Kocha Nathan Jones
Image: TWITTER// SOUTHAMPTON

Klabu ya Southampton imethibitisha uteuzi wa Nathan Jones kama meneja wao mpya baada ya kutimuliwa kwa Ralph Hasenhuttl.

Jones, 49, ameondoka kwenye klabu ya Championship ya Luton Town na kuchukua jukumu hilo kwa kandarasi ya miaka mitatu unusu.

"Ninajivunia sana kupewa nafasi hii," alisema Jones.

Aliongeza, "Ninajua mengi kuhusu klabu tangu zamani za The Dell, hadi kuja hapa St Mary's, na ni klabu nzuri ya soka."

Raia huyo wa Wales atasaidiwa na Chris Cohen na Alan Sheehan ambao wahadumu kama makocho wa kikosi cha kwanza. 

Southampton ilithibitisha kutimuliwa kwa Ralph siku ya Jumatatu na kusema inahisi kuwa sasa ni wakati mwafaka wa mabadiliko.

"Kila mtu anayehusika na klabu angependa kutoa shukrani zao za dhati kwa Ralph kwa jitihada zake zote, pamoja na kujitolea kwake bila kuyumbayumba katika muda wake wote kama meneja," taarifa ya klabu hiyo ilisoma.

Hasenhuttl ,55, aliondoka katika klabu hiyo baada ya kuhudumu kama meneja mkuu kwa takriban miaka minne.

Kocha mkuu wa kikosi cha kwanza cha klabu hiyo, Ruben Selles, alichukua usukani kutoka kwa Ralph kwa muda huku klabu ikitafuta mridhi.

Kutimuliwa kwa Ralph kulitokea masaa machache tu baada ya Southampton kupokea kichapo cha 1-4 kutoka kwa Newcastle.

Klabu hiyo imekuwa ikiandikisha msururu wa matokeo hafifu msimu huu huku ikiwa imejizolea pointi 12 katika mechi 12 ambazo imecheza kufikia sasa.

Jukumu la kwanza la Jones litakuwa wikendi hii ambapo The Saints watasafir hadi ugani Anfield kumenyana na Liverpool.