Kocha wa timu ya Simba SC akamatwa na dawa za kulevya za Heroine

Taarifa hizi zilidhibitishwa na Kamanda Jenerali wa kitengo cha kupambana na dawa za kulevya Tanzania.

Muhtasari

• Akizungumza na wanahabari, kamishna Kasaya alisema Sultan alikamatwa pamoja na wengine tisa ambao walikuwa na kilo zaidi ya 30 za dawa za Heroine.

Kocha wa makipa wa Simba SC
Kocha wa makipa wa Simba SC
Image: Maktaba

Habari za hivi punde kutoka nchini Tanzania zinasikitisha wapenzi wa mchezo wa soka ambapo imearifiwa kocha wa walinda lango wa timu ya Simba nchini humo ametiwa mbaroni baada ya kupatikana na dawa za kulevya aina ya heroine.

Kulingana na vyombo vya habari vilivyosambaza habari hizo Jumanne asubuhi, kocha huyo kwa jina Muharami Said Sultan alitiwa alikamatwa na idara ya kudhibiti matumizi mabaya ya dawa za kulevya na kamishna jenerali Gerald Kasaya alinukuliwa akidhibitisha hilo kwenye vyombo vya habari.

Akizungumza na wanahabari, Kasaya alisema Sultan alikamatwa pamoja na wengine tisa ambao walikuwa na kilo zaidi ya 30 za dawa za Heroine.

“Muharami, kazi anayofanya yeye ni kocha wa timu maarufu jijini Dar es Salaam na Tanzania iitwayo Simba SC. Huyu kocha nafasi yake kubwa ni kocha wa makipa, lakini pia aliwahi kuwa mchezaji wa timu ya Simba,” Kasaya aliwaambia wanahabari.

Kamishna jenerali huyo alidhibitisha kwamba kuanzia mwishoni mwa mwezi uliopita na mwanzoni mwa mwezi Novemba, wamekuwa wakishirikiana kwa ukaribu na vyombo vingine vya usalama katika kuendesha operesheni ambayo imeleta tija ya kuwezesha kukamatwa kwa kilo 34.29 za heroine pamoja na biskuti 50 zilizotengenezwa kwa kutumia bangi ambayo ilitumiwa kama malighafi katika kuunda peremende hizo.

Baada ya haya kuwekwa wazi, sasa inasubiriwa taarifa rasmi kutoka kwa timu ya Simba kuhusu tope hili kubwa ambalo imepakwa baada ya kocha wao wa safu ya langoni kupatikana na dawa hizo za heroine.