Picha ya Ronaldo yaondolewa Old Traford na dondoo zingine za soka ulaya

Picha hiyo iliondolewa saa chache kabla ya mahojiano ya mchezaji huyo na Piers Morgan kupeperushwa siku ya Jumatano.

Muhtasari

• Ronaldo aliweka wazi kuwa hamheshimu meneja  Erik teg Hag,  kwani pia yeye  hajaonyesha heshima kwake.

Mkuu wa klabu ya Sporting Lisbon Frederico Varandas amekanusha ripoti zinazohusisha klabu hiyo ya Ureno na ununuzi wa Cristiano Ronaldo, 37.

Varandas alisema kwamba dau la kumnunua fowadi huyo wa Manchester United na Ureno halijajadiliwa kamwe na kutaja habari hizo kama tu uvumi.

Huku hayo yakijiri uhasama baina ya Ronaldo na Manchester United unazidi kuzagaa baada ya picha ya mchezaji huyo kuripotiwa  kuondolewa nje ya uwanja wa Manchester United, Old Trafford.

Picha hiyo iliondolewa saa chache kabla ya mahojiano ya mchezaji huyo na Piers Morgan kupeperushwa  siku ya Jumatano. 

Klabu ya Manchester United ilitoa taarifa baada ya mshambulizi wake Christiano Ronaldo kuibua madai mazito dhidi yake.

Image: WILLIAM WANYOIKE

Siku ya Jumapili, mwanahabari Piers Morgan alitoa mahojiano na mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno ambapo alilalamikia hali ya klabu hiyo na kuweka wazi kuwa hana furaha tena katika Old Trafford.

United imesema inafahamu kuhusu mahojiano hayo na kutangaza itazingatia jibu lake baada ya ukweli wote kuthibitishwa.

"Lengo letu linasalia katika kujiandaa kwa kipindi cha pili cha msimu na kuendeleza kasi, imani na umoja unaojengwa miongoni mwa wachezaji, meneja, wafanyakazi na mashabiki," taarifa iliyotolewa Jumatatu jioni ilisoma.

Katika sehemu ndogo ya mahojiano ya Morgan na Ronaldo, mshambulizi huyo alidai kuwa baadhi ya watu katika uongozi wa Manchester United akiwemo meneja Erik Ten Hag  wamekuwa wakijaribu kumtimua tangu msimu uliopita, jambo ambalo linamfanya ahisi kusalitiwa.

Aidha aliweka wazi kuwa hamheshimu meneja  Erik teg Hag,  kwani pia yeye  hajaonyesha heshima kwake.

"Simheshimu Erik ten Hag kwa sababu haonyeshi heshima kwangu. Ikiwa huniheshimu, sitawahi kukuheshimu," alisema.

Kwingineko, mazungumzo ya kandarasi kati ya kiungo wa kati wa Uingereza Mason Mount, 23, na wamiliki wa Chelsea yanaendelea na mafanikio yamepatikana "katika wiki chache zilizopita".  

Mason Mount
Mason Mount

Wakati huo huo kukiri kwa Eden Hazard kwamba huenda akaondoka Real Madrid mwezi Januari kunaweza kuwa habari njema kwa Newcastle United, ambayo hapo awali ilihusishwa na kutaka kumnunua kiungo huyo wa kati wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 31.