Ghanim Al-Muftah: Kijana mashuhuri kutoka Qatar aliyeongoza sherehe za ufunguzi wa kombe la dunia

Alipewa miaka michache ya kuishi na wataalamu wa afya, wengi wakisema hawezi kuzidi miaka 15.

Muhtasari

• Kabla ya kuzaliwa kwake, mama yake alishauriwa, mimba yake itolewe ili kuwaondolea wazazi kadhia na mateso ya kuishi na mtoto mwenye hali adimu ya kiafya.

• Sasa ana miaka 20, yu hai na ni miongoni mwa vijana mashuhuri kutoka Qatar.

GHANIM AL-MUFTAH
GHANIM AL-MUFTAH

Ghanim Al-Muftah alizaliwa Mei 5 mwaka 2002. Ni mtoto aliyezaliwa mapacha, yeye na kaka yake.

 Wakati kaka yake akiwa mzima wa afya, yeye alizaliwa na ugonjwa adimu unaojulikana kama Caudal Regression Syndrome (CDS), Ugonjwa ambao huharibu maendeleo ya mgongo wa chini.

Alipewa miaka michache ya kuishi na wataalamu wa afya, wengi wakisema hawezi kuzidi miaka 15.

 Lakini sasa ana miaka 20, yu hai na ni miongoni mwa vijana mashuhuri kutoka Qatar.

GHANIM AL-MUFTAH
GHANIM AL-MUFTAH

Historia ya utoto wake

 Kabla ya kuzaliwa kwake, kwa mujibu wa wakfu wa Ghanim Al-Muftah, mama yake alishauriwa, mimba yake itolewe ili kuwaondolea wazazi kadhia na mateso ya kuishi na mtoto mwenye hali adimu ya kiafya.

 Kwa ujasiri, wazazi wa Ghanim walipingana na ushauri huo na walikubali kuwa hapo ili kumsaidia wakati wote "Nitakuwa mguu wake wa kushoto na wewe utakuwa mguu wake wa kulia". Mama yake alisema.

Ghanim alipokuwa akikua, aliona vigumu kuhudhuria shule hapo awali kwa sababu ya dhihaka na uonevu kutoka kwa wanafunzi wenzake. Hata hivyo, mama yake alimtia moyo kuzungumza na wanafunzi wenzake hao, kuwafundisha kuhusu hali yake, na kuhamasisha jamii.

Mbali ya hali ya kiafya, Ghanim anapenda sana kushiriki michezo mbalimbali
Mbali ya hali ya kiafya, Ghanim anapenda sana kushiriki michezo mbalimbali
Image: GHANIM AL-MUFTAH

Safari ya ujasiriamali

 Ghanim Al-Muftah ni miongoni mwa wajasiriamali wadogo zaidi wa Qatar, anayesherehekea mafanikio yake na kupanua biashara yake. Kwa msaada wa wazazi wake, Ghanim alizindua kampuni ya kutengeneza ‘Ice cream’ (Gharissa Ice Cream), kampuni iliyoko Qatar inayounda uzoefu wa aiskrimu ya nyota tano.

 Ana matumaini kupanua wigo wa kampuni hiyo maarufu hadi katika eneo lote la Ghuba.

 Kwa Ghanim, kuwa mjasiriamali huvuka na kwenda zaidi ya uundaji wa kampuni moja au kadhaa. Anatoa taswira ya mawazo ya kibunifu ambayo yanahusisha kukubali hatari, na kusisitiza kuendeleza katika uundaji wa kazi za baadaye, licha ya vikwazo, hii ndiyo inafafanua roho ya ujasiriamali ya Ghanim.

 Kijana huyu anaamini kwamba "shughuli za ujasiriamali zinapofanywa miongoni mwa vikundi vilivyo hatarini zaidi katika soko la ajira, athari ya kuzidisha thamani hii inawekwa wazi katika jamii kwa ujumla, na katika mkusanyiko wa watu wenye ulemavu haswa"

Ghanim akiwa na pacha wake Ahmad Al Muftah
Ghanim akiwa na pacha wake Ahmad Al Muftah
Image: GHANIM AL-MUFTAH

Kupenda michezo, hadi kuwa balozi wa kombe la dunia 2022

 Licha ya ulemavu wake, Ghanim anapenda kushiriki katika michezo kama kuogelea, kupiga mbizi kwenye barafu, kandanda, kupanda mteremko na kuteleza kwenye barafu.

 Kwa kushangaza, Ghanim amepanda Jebel Shams, kilele cha mlima mrefu zaidi katika eneo lote la Ghuba. Bila woga, ametangaza hadharani nia yake ya kupanda Mlima Everest.

 Kujihusisha na shughuli hizi za kimichezo na harakati zake za kutetea haki za walemavu, hatimaye alichaguliwa kuwa balozi wa kombe la dunia huko Qatar 2022.

 Katika sherehe za ufunguzi wa kombe la dunia 2022, alikua kando ya muigizaji mashuhuri wa Marekani Morgan Freeman.

Image: GHANIM AL-MUFTAH/ TWITTER

Alitoa hutba iliyogusa mioyo ya wengi ulimwenguni. Watu mbalimbali walitoa maoni yao kwenye mitandao ya kijamii, wakisifia ujasiri wa kijana huyu.

Hata hivyo kila mwaka anapatiwa matibabu ya kitaalamu kutoka na hali yake. lakini hilo halijakatisha ndoto zake

 Akiwa na wafuasi zaidi ya milioni 1 kwenye Instagram, Al-Muftah analenga kusoma Sayansi ya Siasa katika chuo kikuu, kwa lengo la kuwa Waziri Mkuu wa baadaye wa Qatar.