Manchester United kuuzwa, Familia ya Glazers yadhibitisha

Taarifa hiyo ilichapishwa kwenye wavuti rasmi wa timu ya Manchester United.

Muhtasari

• Bodi itazingatia njia mbadala zote za kimkakati, ikijumuisha uwekezaji mpya katika klabu, mauzo, au miamala mingine inayohusisha Kampuni - Glazers walisema.

Glazers watangaza kuuza manchester United
Glazers watangaza kuuza manchester United
Image: Getty Images, Facebook

Uongozi wa klabu ya Manchester United wametangaza mipango ya kuuzwa kwa klabu hiyo hivi karibuni kama njia moja ya kuboresha matokeo na mapato ya wawekezaji wake.

Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa kupitia tovuti ya Manchester United, walisema kuwa bodi ya uongozi imeanza kuratibu mipango ya kimkakati itakayonuia kukuza klabu hiyo, kwa lengo la kuiweka United katika nafasi nzuri ya kuwa bora ndani na nje ya uwanja.

“Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni inaanza mchakato wa kutafuta mbinu mbadala za klabu. Mchakato huo umeundwa ili kuimarisha ukuaji wa siku za usoni wa klabu, kwa lengo kuu la kuweka klabu kuchangamkia fursa uwanjani na kibiashara,” taarifa hiyo ilisoma kwa sehemu.

 Katika taarifa hiyo, uongozi ulisema kuwa baadhi ya mikakati hiyo inayofikiriwa ni kuuzwa kwa klabu hiyo na pengine kukubalia wawekezaji wapya kuchukua hisa.

“Kama sehemu ya mchakato huu, Bodi itazingatia njia mbadala zote za kimkakati, ikijumuisha uwekezaji mpya katika klabu, mauzo, au miamala mingine inayohusisha Kampuni. Hii itajumuisha tathmini ya mipango kadhaa ya kuimarisha klabu, ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa viwanja na miundombinu, na upanuzi wa shughuli za kibiashara za klabu katika kiwango cha kimataifa, kila moja katika muktadha wa kuongeza mafanikio ya muda mrefu ya klabu ya wanaume, wanawake, timu ya akademi, na kuleta manufaa kwa mashabiki na wadau wengine,” taarifa ilisema.

Wenyeviti Wenza Watendaji na Wakurugenzi, Avram Glazer na Joel Glazer walisema kuwa wametoa amri ya uongozi wote kutathmini njia zote mbadala za kuhakikisha kwamba hatua yoyote haitawafungia nje mashabiki na wafuasi wa klabu hiyo wapatao bilioni 1.1 kote duniani.

“Tunapotafuta kuendelea kuendeleza historia ya mafanikio ya Klabu, Bodi imeidhinisha tathmini ya kina ya njia mbadala za kimkakati. Tutatathmini chaguzi zote ili kuhakikisha kwamba tunawatumikia mashabiki wetu vyema zaidi na kwamba Manchester United inaongeza fursa muhimu za ukuaji zinazopatikana kwa Klabu leo ​​na katika siku zijazo. Katika mchakato huu wote tutaendelea kulenga kikamilifu katika kutumikia maslahi ya mashabiki wetu, wanahisa, na wadau mbalimbali.”