FIFA yaondoa marufuku dhidi ya shirikisho la soka nchini FKF

Marufuku hiyo iliwekwa mwaka jana, kufuatia serikali kuingilia shughuli za soka nchini.

Muhtasari

• Baada ya kuondoa adhabu hiyo, ujumbe wa FIFA-CAF utatumwa Nairobi ili kufafanua hatua zinazofuata za FKF na kukutana na waziri mpya wa michezo.

Waziri wa Michezo Kenya Ababu Namwamba na mkuu wa Fifa
Waziri wa Michezo Kenya Ababu Namwamba na mkuu wa Fifa
Image: Sports Brief Kenya

Shirikisho la soka duniani FIFA limeondoa marufuku kwa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), chombo kinachosimamia soka nchini Kenya.

Marufuku hiyo iliwekwa mwaka jana, kufuatia serikali kuingilia shughuli za soka nchini, kwa madai ya rushwa na ubadhirifu wa fedha.

Katika taarifa ya Katibu Mkuu wa FIFA, Fatma Samoura, kufuatia kuondolewa kwa marufuku hiyo, bodi hiyo ya kimataifa itatuma wawakilishi kutoka FIFA na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kukutana na waziri mpya wa Michezo Ababu Namwamba.

"Ofisi ya Baraza iliamua mnamo Novemba 25 kuondoa kusimamishwa kwa FKF mara moja," taarifa ya Samoura inasomeka kwa sehemu.

"Baada ya kuondoa adhabu hiyo, ujumbe wa FIFA-CAF utatumwa Nairobi ili kufafanua hatua zinazofuata za FKF na kukutana na waziri mpya wa Michezo,"

Taarifa hizi zinakuja wiki moja tu baada ya waziri Namwamba kufichua kwamba kwa muda mrefu wamekuwa na mazungumzo ya kina na wakuu wa FIFA kuhusu kuondolewa kwa marufuku hiyo.

"Tumekuwa na mazungumzo na Fifa na nina furaha kwamba mambo yanaendelea vyema. Katika mazungumzo yangu ya mwisho na Fifa, nilipata uthibitisho kwamba kusimamishwa kumeondolewa kabisa. Tunasubiri uthibitisho rasmi kwa hilo” Namwamba alisema.

"Michezo imetangaza nchi kwa njia isiyo na kifani. Bendera yetu huinuliwa katika sehemu mbalimbali za dunia, na unahisi fahari ya taifa. Tunataka kumiliki nafasi ya thamani ya michezo kuleta chapa ya Kenya na utambuzi wa chapa hiyo,” Namwamba alisema.