Ronaldo atukanwa mitandaoni kwa kutaka kuhesabiwa bao la Fernandes

Bao hilo lenye utata lilifungwa dakika ya 54 na mwanzo lilihesabiwa Ronaldo lakini baada ya tathmini ya muda ikabainika ni la Fernandes.

Muhtasari

• Tukio hilo lilitokea wakati Ureno ilipomenyana na Uruguay katika Kundi H Kombe la Dunia Jumatatu usiku, Novemba 28.

Ronaldo ashambuliwa kwa kujaribu kumuibia Fernandes bao
Ronaldo ashambuliwa kwa kujaribu kumuibia Fernandes bao
Image: Twitter

Mashabiki wa mchezo wa kandanda na haswa wanaofuatilia kwa ukaribu mashindano ya kombe la dunia yanayoendelea nchini Qatar wamemlimbikizia kiungo mshambuliaji wa Ureno Christiano Ronaldo lawama na kashfa kwa kujaribu kuhesabiwa bao ambalo lilifungwa na kiungo Bruno Fernandes.

Tukio hilo lilitokea wakati Ureno ilipomenyana na Uruguay katika Kundi H Kombe la Dunia Jumatatu usiku, Novemba 28.

Ronaldo na Fernandes walicheza kwa ushirikiano mkubwa uwanjani na kujihakikishia nafasi ndani ya hatua ya 16 bora baada ya kuinyuka Uruguay mabao mawili kwa nunge, mabao yote yalitiwa wavuni na kiungo huyo wa Manchester United, Bruno Fernandes.

Bao la kwanza lilifungwa mwanzoni wa kipindi cha pili baada ya Fernandes kupiga mzinga kimo cha nungunungu aliyekomaa na kutua wavuni.

Wakati mpira huo unaelekea wavuni, Ronaldo alionekana akiruka juu kama kujaribu kuparaza mpira huo lakini hakuufikia na moja kwa moja ulielekea wavuni.

Ronaldo alionekana akionesha ishara kwa muamuzi kuwa bao hilo alilifunga yeye baada ya kupiga kichwa kwa kuparaza lakini mwamuzi alikataa na kumhesabia Fernandes bao hilo.

Tukio hili limemtupa Ronaldo chini ya basi mwendokasi dhidi ya wafuatiliaji wa soka ambao wamemshtumu kwa kujaribu kumuibia Fernandes bao lake.

“Ronaldo hana aibu sana anajifanyaje kuwa ni bao lake wakati anajua kuna mechi za marudio,” mmoja alimkaripia kwenye Twitter.

“Kiuhalisia hata haukumgusa Ronaldo; hilo ndilo lengo la Bruno. Hana aibu jinsi anavyokimbia kusherehekea na kudai,” mwingine alisema.