Kombe la Dunia: Tazama ratiba ya robo fainali

Mechi ya mwisho ya hatua ya mwondoano ilichezwa Jumanne usiku.

Muhtasari

•Nchi ya Morocco ilifuzu kwa hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia.

•Ureno kupata ushindi mkubwa wa 6-1 dhidi ya washindani wao katika raundi ya mwondoano.

Mlinda lango wa Morocco Yassine Bounou aliibuka bingwa katika mechi yao dhidi ya Uhispania.
Image: HISANI

Mashindano ya Kombe la Dunia sasa yameingia raundi ya robo fainali baada ya mechi ya mwisho ya hatua ya mwondoano kuchezwa Jumanne usiku.

Siku ya mwisho ya hatua ya mwondoano ilishuhudia Morocco ikifuzu kwa robo fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia.  Taifa hilo la kaskazini mwa Afrika iliwabwaga mabingwa wa Kombe la Dunia mwaka wa  2010,  Uhispania katika hatua ya mikwaju ya penalti baada ya mechi kuisha 0-0 baada ya muda wa ziada.

Abdelhamid Sabiri, Hakim Ziyech na Achraf Hakimi walifunga penalti tatu za Morocco huku Uhispania wakishindwa kufunga penalti yoyote kati ya tatu ambazo walipiga. Mlinda lango Yassine Bounou aliibuka bingwa wa mchuano huo.

Morocco sasa itachuana na Ureno katika robo fainali mnamo Jumamosi, Desemba 10. Hii ni baada ya Ureno kupata ushindi mkubwa wa 6-1 dhidi ya washindani wao katika raundi ya mwondoano, Uswizi. Goncalo Ramos (3), Pepe, Raphael Guerreiro na Rafael Leao ndio waliofanikisha ushindi wa Ureno huku beki Manuel Akanji akifungia Uswizi bao la pekee la kufuta machozi.

Timu zingine ambazo zilikuwa zimefuzu awali ni Brazil na Croatia ambazo zitamenyana mnamo Desemba 9, Uholanzi na Argentina ambazo zitachuana siku hiyo hiyo pamoja Uingereza na Ufaransa ambao watamenyana Desemba 10.

Tazama ratiba ya michuano ya robo fainali hapa:-

1. Croatia vs Brazil - Ijumaa, Desemba 9 (6PM)

2. Uholanzi vs Argentina- Ijumaa, Desemba 9 (10PM)

3. Morocco vs Ureno - Desemba 10 (6PM)

4. Uingereza vs Ufaransa - Desemba 10 (10PM)